Jumanne, 24 Septemba, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 20 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1446 Hijria sawa na tarehe 24 Septemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 996 iliyopita yaani tareher 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 450 Hijria, alifariki dunia Abu Tayyib Tabari, faqihi na mwandishi wa Kiislamu huko Baghdad.
Abu Tayyib alizaliwa mwaka 348 Hijria huko Amol, moja kati ya miji ya kaskazini mwa Iran. Tabari alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa lengo la kutafuta elimu. Abu Tayyib Tabari, aliishi na kufundisha huko Baghdad ambapo alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa za zama zake. Faqihi Tabari alikuwa hodari katika taaluma ya fasihi na utunzi wa mashairi.
Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Jawab fi al Sima'a" na "al Ghinaa wa al Ta'aliqatil Kubra fil Furu'u.

Katika siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, ndege za kijeshi za Ujerumani zilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya mji mkuu wa Poland, Warsaw.
Mashambulio hayo yalifanyika sambamba na kuanza Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na yaliendelea kwa muda wa siku tatu. Hatimaye wananchi wa mji huo walisalimu amri mbele ya majeshi ya Ujerumani baada ya mapambano na siku kumi na moja.
Mashambulio hayo ya kinyama yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 15,000.

Katika siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, Guinea Bissau ilitangaza uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mreno.
Guinea Bissau iligunduliwa mwaka 1446 na Mwana Mfalme Henry aliyekuwa akitawala Ureno pamoja na wenzake na kuwa koloni la nchi hiyo. Guinea Bissau ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Guinea Ureno, ilikuwa miongoni mwa vituo vya biashara ya utumwa ya wazungu katika karne za 17 na 18.
Na hatimaye ilipofika mwaka 1974, Ureno ikakubali kuwa huru nchi ya Guinea Bissau. Guinea Bissau iko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Atlantic.
