Ijumaa, Septemba 27, 2024
Leo ni Ijumaa tarehe 23 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na 27 Septemba 2024 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1245 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Bibi Fatma Maasuma dada wa Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as) aliwasili katika mji wa Qum, Iran.
Mwaka mmoja baada ya safari ya kubaidishiwa kaka yake huko katika mji wa Marv, Bibi Maasuma alifunga safari kutoka Madina kwa ajili ya kwenda kuonana na kaka na Imam wake huko Khorasani. Baada ya kuwasili Qum, aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (saw). Mwishowe tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake Imam Ridha (as), Bibi Fatima Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa.
Hii leo Haram ya mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw), Bibi Fatma Maasuma (as) katika mji wa Qum ni moja ya maeneo matakatifu ambapo watu kutoka katika maeneo mbalimbali ya dunia huenda kufanya ziara katika eneo hilo.

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, mji wenye jamii kubwa ya watu wa Beijing ulichaguliwa rasmi kuwa mji mkuu wa Uchina.
Mji wa kihistoria wa Beijing unapatikana mashariki mwa nchi hiyo na unahesabiwa kuwa moja ya vituo vikubwa vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni nchini China.
Beijing ilichaguliwa kuwa mji mkuu wa China baada ya Mao Tse-tung kuchukua madaraka ya nchi na kiongozi wa wakati huo wa China Chiang Kai-shek kulazimika kukimbilia Taiwan.
Tarehe 27 Septemba inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya Utalii.
Utalii ni moja ya sekta muhimu za mabadilishano ya kiutamaduni baina ya watu wa mataifa mbalimbali. Aidha utalii unaweza kutimia kupitia safari na utalii wa ndani na nje ya nchi kwa madhumuni tofauti.
Licha ya kwamba utalii umekuwa na historia ya muda mrefu katika maisha ya mwanadamu, lakini utalii wa mfumo wa kisasa ulianza mwanzoni mwa karne ya 16, wakati yaliposhika kasi mapinduzi ya kiviwanda barani Ulaya na kuvumbuliwa aina mpya ya maisha barani humo. Ni kuanzia karne ya 17 ndipo istilahi ya utalii ilipoenea zaidi hasa katika jamii ya watu wa Ufaransa.
