Alkhamisi, tarehe 26 Septemba, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 22 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na Septemba 26, 2024.
Siku kama ya leo miaka 1442 iliyopita, yaani tarehe 22 Rabiul-Awwal mwaka wa 4 Hijiria, kulianza vita kati ya Waislamu na Mayahudi wa kabila la Bani Nadhir baada ya watu wa kabila hilo kufanya njama za kutaka kumuua Mtume Muhammad (saw).
Bani Nadhir ni moja ya makundi matatu ya Mayahudi waliokuwa wakiishi katika vitongoji vya mji wa Madina, ambao kwa mujibu wa mkataba waliotiliana saini na Mtume (SAW), hawakutakiwa kuchukua hatua yoyote iliyo dhidi ya mtukufu huyo na Waislamu kwa ujumla.
Baada ya Mayahudi kuvunja mkataba huo, Mtume Muhammad (SAW) aliwaamuru waondoke Madina. Hata hivyo Mayahudi hao ambao tayari walikuwa wamepewa ahadi za kuungwa mkono na wanafiki wa mji huo, hawakuwa tayari kutii amri hiyo. Ni kwa sababu hiyo, ndipo mtukufu Mtume kwa kushirikiana na Waislamu akazizingira ngome za watu hao kwa muda wa siku kadhaa na kuwalazimisha kuondoka katika maeneo yao.
Katika siku kama ya leo miaka 136 iliyopita alizaliwa Thomas Stearns Eliot mshairi na mwanafasihi mashuhuri wa Uingereza.
Malenga huyo ambaye ni mashuhuri kwa jina la S. T. Eliot alitoa nudhumu yake ya kwanza ya mashairi mwaka 1922 iliyokuwa na jina la "The Waste Land" na kupata umashuhuri mkubwa. Mwanafasihi huyo wa Kiingereza aliaga dunia mwaka 1965.
Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1907, nchi ya New Zealand iliyoko mashariki mwa Australia ilipata uhuru.
Visiwa vya New Zealand vilikoloniwa na Uingereza mwaka 1769 na karne ya 19, ilishuhudia ukoloni dhidi ya nchi hiyo ukishadidi sambamba na wimbi kubwa la wahajiri wa Kiingereza waliokuwa wakielekea katika nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1960, Makamu wa Rais wa Marekani Richard Nixon na Seneta John F.
Kennedy wa Massachusetts walikabiliana katika mdahalo wa kwanza wa televisheni wakati wakiwania tiketi ya kuingia ikulu ya White House. John Kennedy aliibuka na ushindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka huo. ***
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita wapiganaji shujaa wa Iran walifanikiwa kuvunja mzingiro wa mji wa Abadan katika operesheni ya haraka na iliyokuwa imeratibiwa vyema dhidi ya ngome za jeshi la Saddam Hussein wa Iraq.
Operesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji wa Iran kufuatia agizo la kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu.
Mji wa Abadan ulikuwa umezingirwa na wanajeshi wa Iraq kwa karibu mwaka mmoja tangu kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa dikteta Saddam dhidi ya Iran.

Na siku kama hii ya leo miaka 12 iliyopita Maya Nasri mwandishi habari wa Kikristo wa kanali ya televisheni ya Press ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa mjini Damascus nchini Syria wakati alipokuwa akitayarisha ripoti kwa ajili ya kanali hiyo. Maya Nasr alizaliwa tarehe 30 Julai mwaka 1979 nchini Syria na kuhitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Kaplan kilichoko New York huko Marekani. Nasr akiwa pamoja na Mkurugenzi wa kanali ya televisheni ya Press nchini Syria, Hussein Murtadha, alishambuliwa kwa kupigwa risasi mbili kichwani na mlenga shabaha wa wapinzani wa serikali ya Damascus wakitayarisha ripoti ya matukio ya Syria. Mwenzake Maya, Hussein Murtadhaa alijeruhiwa katika shambulizi hilo.