Jumapili, 29 Septemba, 2024
Leo ni Jumapili 25 Mfunguo Sita Rabiu Awwal 1446 Hijria m,wafaka na 29 Septemba 2024 Miladia.
Siku ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, yaani tarehe 8 Mehr, ni maarufu hapa nchini Iran kama siku ya kumuenzi Maulana Jalaluddin Balkhi maarufu kwa jina la Moulavi. Maulana Jalaluddin alizaliwa mwaka 604 Hijria Qamaria katika mji wa Balkh uliokuwa moja kati ya miji ya Iran ya kipindi hicho. Moulavi alikuwa gijwi wa mashairi na malenga mwenye uwezo na kipaji kikubwa katika karne ya 7 Hijria. Miongoni mwa athari kubwa za Maulana au Jalaluddin Balkhi ni kitabu cha mashairi cha Masnavi Maanavi. ***
Katika siku kama ya leo miaka 1010 iliyopita sawa na tarehe 25 Rabiul Awwal mwaka 436 Hijiria alifariki dunia Sayyid Murtadha Alamul Huda mwanafunzi mashuhuri wa Sheikh Mufid. Alizaliwa mwaka 355 Hijiria huko Baghdad na alijifunza elimu za zama zake. Baadaye alianzisha kituo cha elimu ambacho kilikuwa kikihudhuriwa na watu wenye itikadi na mielekeo tofauti. Sayyid Murtadha ameacha vitabu vingi na miongoni mwa vitabu hivyo ni Tanzihil Anbiyah, Taqribul Usul pamoja na kitabu cha maashairi chenya beti elfu 20. ***
Miaka 123 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mwanafizikia mashuhuri wa Italia, Enrico Fermi katika mji wa Roma. Baada ya kukamilisha masomo ya chuo kikuu alivumbua Kanuni ya Mwendo wa Molekuli ya Gesi. Fermi alifanya uchunguzi kuhusu mabadiliko ya atomu na akafanikiwa kutengeneza betri ya atomu kwa kuipasua na kutoa nje nishati yake. Mwanafizikia huyo wa Italia alifariki dunia mwaka 1954. ***
Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, alifariki dunia mwandishi wa Kifaransa, Emile Zola. Zola alizaliwa mjini Paris mwaka 1840. Zola alindika vitabu vingi katika elimu tofauti. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwandishi huyo wa Ufaransa ni "Therese Raquin” "Nana", "The Belly of Paris na "Germinal."