Oct 05, 2024 02:22 UTC
  • Jumamosi, 5 Oktoba, 2024

Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria ambayo inasadifiana na 5 Oktoba 2024.

Katika siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, alizaliwa Louis Jean Lumiere, mwanakemia mashuhuri wa Kifaransa. Mwaka 1895 akiwa pamoja na ndugu yake aliyejulikana kwa jina la Auguste Lumiere, walifanikiwa kutengeneza kifaa ambacho kiliwasaidia kuchukua picha mbalimbali na kusajili harakati. Mwaka huo huo Lumiere alifanikiwa kuonyesha filamu yake ya kwanza au Motion Picture katika majumba ya sinema.  ***

Louis Jean Lumiere

 

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Slobodan Milosevic dikteta wa zamani wa Yugoslavia na mhusika mkuu wa vita vya umwagaji damu huko Balkan, alijiuzulu baada ya miezi kadhaa ya malalamiko ya ndani na vikwazo vya kimataifa. Milosevic alikuwa rais wa Serbia tangu mwaka 1990 hadi 1997 na baadaye akawa Rais wa Jamhuri ya Yugoslavia. Katika vita vya Bosnia, na kwa uungaji mkono wa kila upande wa Waserbia, Slobodan Milosevic alishiriki pakubwa katika kutekeleza mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Milosevic alikuwa kiongozi wa kwanza mtenda jinai za kivita kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa kwa ajili ya kuhukumiwa. Hata hivyo mhalifu huyo katili alifariki dunia akiwa katika korokoro za mahakama hiyo huko The Hague nchini Uholanzi kutokana na mwendo wa kinyonga wa kushughulikia kesi yake. 

Slobodan Milosevic

 

Tarehe 5 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu. Siku hii ilitangazwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika tarehe 3 hadi 8 mwezi Septemba mwaka 1994 kwa ajili ya kuenzi mchango wa walimu na nafasi yao kubwa katika jamii ya mwanaadamu. 

 

Tags