Jumapili, 6 Oktoba 2024
Leo ni Jumapili tarehe Pili Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria ambayo inasadifiana na 6 Oktoba 2024.
Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, Muhammad Ali Shah Qajar alitia saini kikamilisho cha Katiba. Kufuatia kushadidi harakati za kupigania katiba nchini Iran na mapambano ya kila upande ya wananchi na viongozi wa kidini, Mozaffar ad-Din Shah Qajar alilazimika kukubaliana na matakwa ya wananchi ambapo mbali na mambo mengine alitoa amri ya kuundwa Bunge la Taifa. Awali Muhammad Ali Shah alikuwa akipoteza muda katika kufanikisha kikamilisho hicho cha Katiba, lakini mashinikizo ya wananchi na wanazuoni yalimlazimisha katika siku kama ya leo alazimika kutekeleza jambo hilo. ***
Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, Sohrab Sepehri malenga na mchoraji wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Kashan moja ya miji ya katikati mwa Iran. Mwaka 1330 Hijiria Sepehri alitoa majimui ya kwanza ya tungo zake za mashairi zilizoitwa "Marge Rang" na akatoa tena majimui nyingine ya vitabu vinane. Aidha mbali na Sohrab Sepehri kuwa malenga mkubwa, alipendelea sana taaluma ya uchoraji. Miongoni mwa athari za Sepehri ni pamoja na majimui za vitabu vya mashairi vinavyoitwa "Zendegi Khob'ha", "Musafir" na "Aavaz Oftaab." Sohrab Sepehri alifariki dunia mwaka 1359 Hijiria na kuzikwa mahali alipozaliwa yaani mjini Kashan. ***
Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita sawa na tarehe 6 Oktoba mwaka 1973, vilianza vita vya nne kati ya Waarabu na utawala ghasibu wa Israel. Katika siku hiyo jeshi la Misri lilivishambulia vikosi vya utawala huo haramu katika oparesheni ya kushtukiza katika upande wa pili wa Mfereji wa Suez. Baada ya kuvunja mstari imara wa ulinzi wa Barlow, vikosi hivyo vikafanikiwa kuingia katika jangwa la Sinai. Katika vita hivyo vikosi vya majeshi ya Misri na Syria viliyatia hasara kubwa majeshi ya utawala wa Israel na idadi kadhaa ya ndege za kivita za Wazayuni zikasambaratishwa. Hata hivyo kutokana na hatua ya Marekani ya kuupatia silaha za kisasa utawala huo wa Kizayuni, Waarabu walipoteza baadhi ya ushindi waliokuwa wameupata katika vita hivyo.
Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani mwaka 1981 maafisa kadhaa wa kundi la Kiislamu la "Al-Jihad" walishambulia na kumuua rais wa wakati huo wa Misri, Muhammad Anwar Sadat. Rais huyo aliuawa kwa sababu ya kutia saini makubaliano ya udhalilishaji ya Camp David mnamo mwaka 1978 na utawala ghasibu wa Israel sambamba na kuutambua rasmi utawala huo haramu. Kufuatia hatua hiyo rais huyo alihesabiwa kuwa msaliti wa malengo matukufu ya Waislamu na Waarabu. Kwa upande mwingine hatua hiyo ilipelekea kutengwa Misri baina ya nchi za Kiislamu. Ni kwa sababu hiyo ndipo makundi ya Kiislamu na wanamapambano wa Misri wakaamua kumuua Sadat, ambaye alionekana kuwa msaliti mkubwa kwa kuutambua rasmi utawala huo ghasibu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu. Aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa Khalid Islambuli, mmoja wa maafisa wa jeshi la Misri wakati huo.
Na leo tarehe 6 Oktoba Misri ambayo ni moja kati ya tamaduni za kale zaidi duniani ilianzisha serikali ya jamhuri yenye bunge baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Jamhuri ya Kiarabu ya Misri ina siku mbili za taifa ambazo ni tarehe 23 Julai na 6 Oktoba. Tarehe 23 Julai ni siku ya mapinduzi dhidi ya utawala wa kifalme wa Mfalme Faruq hapo mwaka 1952 mapinduzi ambayo yaliandaa uwanja wa kutangazwa jamhuri ya nchi hiyo.