Oct 12, 2024 02:47 UTC
  • Jumamosi, 12 Oktoba, 2024

Leo ni Jumamosi 8 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria mwafaka na 12 Oktoba 2024 Miladia.

Miaka 1214 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 8 Rabiu Thani mwaka 232 Hijria Qamaria, Imam Hassan Askari AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina. Akiwa katika umri wa utotoni, mtoto huyo alilazimishwa na makhalifa wa Bani Abbas akiwa na baba yake Imam Hadi AS, kuondoka mji huo na kuhamia katika mji wa Samarra ambao wakati huo ulikuwa makao makuu ya utawala wao. Japokuwa mtukufu huyo hakuweza kuishi zaidi ya miaka 28 lakini aliacha nyuma maarifa muhimu na adhimu ya Kiislamu.  Imam Hassan Askari AS alikuwa na huruma na upendo mkubwa uliokuwa ukiwavutia watu wengi. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hassan Askary alichukua jukumu zito la kuwaongoza Waislamu sambamba na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu. Kama walivyokuwa Maimamu wengine watukufu, Imam Hassan Askari naye aliitumia karibu sehemu yote ya umri wake kulinda na kueneza mafunzo sahihi na a'ali ya dini tukufu ya Kiislamu. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 1089 iliyopita, Abu Feras Hamdani mshairi na mwandishi wa Kiarabu alifariki dunia. Sambamba na kuwa mshairi, Abu Feras alikuwa mpiganaji vita na alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa Seif al-Daulah mtawala wa Halab na alikuwa mmoja wa makamanda wa jeshi.  ***

Abu Feras Hamdani

 

Katika siku kama hii ya leo miaka 60 iliyopita bunge la kimaonyesho la Iran lilipasisha sheria iliyowapa washauri wa kijeshi wa Marekani nchini kinga ya kutofikishwa mahakamani iwapo wangepatikana na hatia ya aina yoyote (Capitulation Accord) . Kwa mujibu wa sheria hiyo, wahalifu wa Kimarekani wangehukumiwa nchini kwao kama watatenda jinai nchini Iran, na mahakama za Iran hazikuwa na haki ya kushughulikia kesi zao. Sheria hiyo ilitambuliwa kuwa dharau kwa taifa la Iran na iliyokiuka wazi kujitawala kwa nchi. Kwa msingi huo hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) siku kadhaa baada ya kupasishwa sheria hiyo bungeni alitoa hotuba ya kihistoria akieleza taathira zake na kumshambulia vikali Mfalme Shah na Marekani. Baada ya hotuba hiyo Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni.  ***

 

Tarehe 12 Oktoba miaka 25 iliyopita, Jenerali Parviz Musharraf, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Pakistan alifanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa wakati huo wa nchi hiyo Muhammad Nawaz Sharrif. Baada ya mapinduzi hayo Musharraf ambaye alichukua madaraka ya rais wa nchi, alivifanyia mabadiliko baadhi ya vipengee vya katiba ya nchi hiyo na kuzidisha nguvu na uwezo wa rais. Hata hivyo kutokana na kuongezeka mashinikizo ya ndani na nje, Musharraf alisalimu amri mwezi Novemba 2007 na kuachia cheo cha Mkuu wa majeshi ya Pakistan. Musharraf aliondoka kikamilifu madarakani mwezi Julai 2008, baada ya kushika kasi vyama vya upinzani ambavyo vilishinda uchaguzi wa rais.  ***

Jenerali Parviz Musharraf