Oct 19, 2024 02:32 UTC
  • Jumamosi, 19 Oktoba, 2024

Leo ni Jumamosi 15 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria mwafaka na 19 Oktoba 2024 Miladia.

Miaka 243 iliyopita katika siku inayofanana na ya leo, Charles Cornwallis, kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Uingereza nchini Marekani alisalimu amri mbele ya George Washington, kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Marekani na kwa msingi huo vita vya kuikomboa Marekani vikamalizika rasmi. Vita hivyo vilianza mwaka 1775 kati ya wahajiri wa Kimarekani na wakoloni wa Kiingereza. Miaka miwili baada ya ushindi wa mwisho wa wahajiri, pande mbili hizo zilisaini makubaliano mwaka 1783 ambapo kwa mujibu wake Uingereza ilitambua rasmi uhuru wa Marekani. ***

Charles Cornwallis

 

Miaka 205 iliyopita nchi ya Colombia ilijikomboa kikamilifu kutoka katika ukoloni wa Uhispania. Zamani za kale, ardhi ya Colombia ilikuwa makazi ya kaumu mbalimbali. Mwaka 1538 Colombia iliangukia mikononi mwa ukoloni wa Uhispania na kuanzia hapo, ilivamiwa mara nyingi na madola ya kikoloni kama Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo kwa kupita zama harakati za kupigania ukombozi zilichukua wigo mpana nchini humo na kuanzia mwaka 1781 kulianza kushuhudiwa uasi wa kutaka kujikomboa ambao ulikandamizwa vikali. Hata hivyo hatimaye katika siku kama ya leo utawala wa kikoloni wa Uhispania ulisambaratishwa nchini Caolombia.

 

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, Ali Hassan Salameh mmoja kati ya viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliuawa shahidi nchini Lebanon kupitia njama za vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel, MOSSAD. Salameh alikuwa afisa wa usalama wa PLO na aliuawa shahidi baada ya kuripuka bomu lililotegwa katika gari lake mjini Beirut. Jinai hiyo ya utawala haramu wa Israel ndani ya Lebanon kwa mara nyingine iliweka wazi ugaidi na uvamizi wa Israel dhidi ya ardhi ya nchi nyingine. ***

Ali Hassan Salameh

 

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, alifariki dunia Ali Ezzat Begovic, mwanasiasa na mwandishi wa Bosnia Herzegovina. Ali Begovic alizaliwa mwaka 1925 na kupata taaluma ya sheria katika Chuo Kikuu cha Sarajevo katikati mwa Bosnia. Alianza kupambana na utawala wa kikomunisti wa Yugoslavia ya zamani akiwa kijana mdogo na kufungwa jela mara kadhaa. Mwaka 1989 Ali Begovic aliasisi chama kipya cha siasa kwa jina la Democratic Action kilichokuwa na nafasi kubwa katika uhuru wa Bosnia mwaka 1991. Mwanasiasa huyo wa Kiislamu ambaye baada ya uhuru wa taifa hilo alichaguliwa kuwa rais, alikuwa na nafasi kubwa katika kuwatetea raia wa Bosnia katika mashambulizi ya askari wa Serbia dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. 

Ali Ezzat Begovic