Oct 20, 2024 02:44 UTC
  • Jumapili, 20, Oktoba, 2024

Leo ni Jumapili 16 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria mwafaka na 20 Oktoba 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, inayosadifiana na 20 Oktoba 1827 kulitokea vita vya majini katika ghuba ndogo ya Navarone iliyoko kaskazini mwa bahari ya Mediteranean. Kwenye vita hivyo, majeshi ya Uingereza, Russia na Ufaransa ambayo yalikuwa yakiiunga mkono Ugiriki, yakitumia meli za kivita, yalishambulia meli za dola ya Othmania. Nchi hizo tatu za Ulaya ziliangamiza kabisa meli 60 za kivita za dola la Othmania na kuwateka nyara wanajeshi elfu sita. ***

 

Siku kama ya leo miaka 165 iliyopita, alizaliwa John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How we Think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture". John Dewey alifariki dunia mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 92.  

John Dewey

 

Miaka 72 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, Jomo Kenyatta mwanaharakati, mwanasiasa na mpigania uhuru mashuhuri barani Afrika na Rais wa Kwanza wa Kenya alitiwa mbaroni kufuatia amri ya utawala wa kikoloni nchini Kenya. Mzee Kenyatta alikuwa miongoni mwa watu 100 mashuhuri nchini humo waliotiwa mbaroni katika kipindi cha masaa 24 ikiwa ni katika fremu ya mpango wa kuibana Mau Mau, kundi la wapiganaji wa Kenya waliokuwa wakiupinga utawala wa kikoloni wa Waingereza. Wakenya huadhimisha siku hii kama Sikukuu ya Mashujaa na kuwakumbuka wale wote waliopigania uhuru wa taifa hilo. ***

 

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, vibarua na wafanyakazi wa sekta ya mafuta nchini Iran walianza kufanya mgomo wa nchi nzima wakati wa kujiri harakati za mapambano ya wananchi dhidi ya utawala dhalimu wa Shah. Kufuatia mgomo huo, usafirishaji mafuta nje ulisimamishwa, jambo ambalo liliukatia utawala wa Shah moja ya vyanzo muhimu vya kipato. Aidha kusimamishwa usafirishaji mafuta ya Iran nje ya nchi, kulipelekea kupanda mno kwa bei ya bidhaa hiyo ulimwenguni. Utawala wa Shah ulitumia vitisho mbalimbali ili kuwafanya wafanyakazi hao warejee kazini, lakini mgomo huo uliendelea hadi utawala huo kibaraka ulipoangushwa. Wananchi wanampinduzi wa Iran licha ya kukabiliwa na matatizo mengi yaliyosababishwa na uhaba wa nishati ya mafuta, lakini walisimama kidete na kuuunga mkono mgomo wa wafanyakazi hao wa sekta ya mafuta. ***

 

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alikamatwa na wanamapinduzi karibu na mji wa bandari wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa. Gaddafi aliuawa baada ya miezi kadhaa ya mapigano na wanamapinduzi ambapo jeshi lake liliwaua maelfu ya wananchi hususan katika miji ya Benghazi na Tripoli. Gaddafi ambaye aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 42 alizaliwa mwaka 1942. Aliingia madarakani mwaka 1969 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani mfalme Mohammad Idris al-Sanusi. 

Kanali Muammar Gaddafi