Oct 26, 2024 03:08 UTC
  • Jumamosi, 26 Oktoba, 2024

Leo ni Jumamosi 22 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria mwafaka na 26 Oktoba 2024.

Siku kama ya leo miaka 1150 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Musa al-Mubarqa' mtoto wa Imam Muhammad Taqi al-Jawad na ndugu wa Imam al Hadi (as) aliaga dunia katika mji mtakatifu wa Qum, Iran. Alizaliwa Madina mwaka 214 Hijria na mpaka anafikisha umri wa miaka 6 ambapo baba yake aliuawa shahidi, alikuwa chini ya malezi na usimamizi wa baba yake huyo. Baadaye alijifunza elimu kwa kaka yake, yaani Imam al Hadi (as). Musa al-Mubarqa' kipindi fulani aliishi katika mji wa Kufa katika Iraq ya leo na alipokuwa na umri wa miaka 42 alisafiri na kuelekea katika mji wa Qum, Iran. Aliishi Qum akijishughulisha na ulinganiaji wa dini ya Uislamu hadi alipofariki dunia katika siku kama ya leo. Musa al-Mubarqa' ana daraja ya juu ya kielimu na alikuwa mpokezi wa Hadithi. Aidha alisifika mno kwa taqwa na uchamungu. ***

 

 Katika siku kama ya leo miaka 184 iliyopita, alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad Taqi Razi, katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".  ***

 

Miaka 77 iliyopita katika siku kama hii ya leo eneo la kiistratejia la Jammu na Kashimir liliunganishwa na India baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na Pakistan kujitenga na India. Ilipangwa kuwa, eneo la Jammu na Kashmir lenye wakazi wengi Waislamu litajiunga na Pakistan lakini mtawala wa eneo hilo akichochewa na India na Uingereza, aliamua kuliunganisha na India na kupuuza matakwa ya wananchi. Baada ya kutangazwa habari hiyo Pakistan ililishambulia eneo hilo na kutwaa sehemu ya Jammu na Kashmir. Tangu wakati huo hadi sasa India na Pakistan zimepigana vita mara mbili juu ya umiliki wa eneo la Jammu na Kashmir na hitilafu za pande hizo mbili zingali zinaendelea. ***

 

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani, alimu mkubwa na mtaalamu wa elimu ya fiqhi. Ayatullah Zanjani alizaliwa mwaka 1308 Hijiria, huku akisomea elimu ya awali na ya juu mjini Zanjan. Baada ya hapo alielekea mjini Qum kwa ajili ya kuendelea na elimu ambapo alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Abdul-Karim Haeri Yazdi na Muhammad Hujjat Kuh-Kamari. Baada ya Ayatullah Muhammad Hujjat kufariki dunia, Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani alichukua wadhifa wa kuswalisha swala ya jamaa katika shule ya Fayzia. Aidha katika muongo wa 1320 Hijiria Shamsia, msomi huyo alikutana na Imam Khomeini (MA) ambapo alishirikiana naye katika vikao vingi vya kielimu. Vitabu kama vime 'Arbain' 'Afwahur-Rijal' 'Furuqul-Ahkaam' na vitabu 20 vingine ni sehemu ya turathi za Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani. ***

 

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita maajenti wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Katibu Mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Dakta Fat'hi Shiqaqi, akiwa huko Malta. Shiqaqi alizaliwa mwaka 1951 katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza. Alihitimu masomo ya udaktari na kufanya kazi katika hospitali moja ya Baitul Muqaddas. Alianzisha harakati za mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel akiwa bado kijana. Mwaka 1979 Dakta Shiqaqi alikamatwa na kusweka jela nchini Misri kwa sababu ya kuandika kitabu kuhusu harakati za Imam Ruhullah Khomeini na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Dakta Shiqaqi aliitangaza Siku ya Kimataifa ya Quds iliyoainishwa na Imam Khomeini, kuwa ni siku ya kuhuisha Uislamu na mapambano ya jihadi dhidi ya Wazayuni huko Palestina. ***

Dakta Fat'hi Shiqaqi,

 

Tags