Nov 01, 2024 02:27 UTC
  • Ijumaa, tarehe Mosi Novemba, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 28 Rabiuthani 1446 Hijria sawa na tarehe Mosi Novemba 2024.

Miaka 808 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Damascus.

Alizaliwa mwaka 560 Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka, Halab (Aleppo) na Baghdad, na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa.

Ibn Arabi alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al-Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".   

Katika siku kama ya leo miaka 534 iliyopita, alizaliwa Mirza Sharaf Jihan Qazvini, mshairi mahiri wa Kiirani.

Alizaliwa katika mji wa Qazvin moja ya miji ya Iran. Alisoma kwa Amir Ghiyath Din mwanazuoni mashuhuri wa zama hizo. Mirza Sharaf Jihan mbali na kubobea katika elimu za akili na nakili na kuzifundisha alikuwa mwalimu pia katika taaluma za fasihi na mashairi. 

Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita utawala wa kifalme nchini Uturuki ulihitimishwa rasmi na Kemal Ataturk.

Baada ya kumalizika kwa Vita vya Kwanza vya Dunia sanjari na kudhoofika na kupoteza ushawishi wa utawala wa Othmania, Atatürk aliamua kuvunja utawala huo wa kifalme na kutwa uongozi. Hata hivyo haikuwa rahisi kwa Mustafa Kemal Atatürk kumaliza utawala wa kifalme wa Othmania ambao ulikuwa na misingi ya kidini.

Hivyo mwanzoni alitenganisha baina ya utawala wa kisultani na cheo cha ukhalifa wa Waislamu na tarehe Mosi mwaka 1922 akavunja rasmi utawala wa kifalme huku cheo cha ukhalifa kikibakia kama cheo cha heshima tu. Suala hilo liliharakisha kuporomoka kwa utawala wa kifalme wa Othmania uliodumu kwa kipindi cha miaka 600.

Baada ya kuporomoka utawala huo, uliundwa utawala wa Jamhuri na wa kisekulari hapo tarehe 29 Oktoba mwaka 1923. 

Kemal Ataturk na Reza Khan

Katika siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, vilianza vita vya ukombozi wa Algeria baada ya kuundwa Harakati ya Ukombozi wa Algeria chini ya uongozi wa Ahmed ben Bella.

Baada ya kupita miaka 132 ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria, hatimaye mwaka 1962 mapambano ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Algeria yalizaa matunda na nchi hiyo kujipatia uhuru wake.

Baada ya kutangazwa uhuru wa Algeria, Ahmed ben Bella alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Utawala wa Ahmed ben Bella ulidumu kwa miaka mitatu tu, kwani ulipofika 1965 alipinduliwa na Kanali Houari Boumediene aliyekuwa waziri wake wa ulinzi.     

Ahmed ben Bella