Nov 22, 2024 02:30 UTC
  • Ijumaa, Novemba 22, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 20 Mfunguo Nane, Jamadil Awwal 1446 Hijria inayosadifiiana na 22 Novemba 2024.

Siku kama ya leo miaka 764 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Jumadil Awwal 682 Hijria, alizaliwa Muhammad bin Hassan Hilli mwenye lakabu ya Fakhrul Muhaqqiqiin katika mji wa Hilla nchini Iraq.

Muhaqqiq Hilli  alibobea na kutabahari kwenye elimu za Tafsiri ya Qur’ani, Fiqh na Usulul Fiqh. Mwanachuoni huyo alipata elimu ya kidini kutoka kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake.

Fakhrul Muhaqqiqiin ameandika vitabu vingi miongoni mwavyo ni "Sharh Mabadiul Usul", "Tahswilul Najat" na “al Kafiya”. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 771 Hijria.   

Mahali lilipo kakburi la Muhammad bin Hassan Hilli  

Siku kama ya leo miaka 709 iliyopita yaani tarehe 20 Jamadil Awwal mwaka 737 alifariki dunia faqihi wa Kiislamu Abu Abdullah Muhammad ibn Hajj al-Abdari al-Fasi mashuhuri kwa jina la Ibn Hajj.

Al Fasi awali alipata elimu kwa maulamaa wa mji wa Fas huko Morocco ya leo. Baadaye alielekea Cairo na kuishi huko hadi mauti yalipomfika. Faqihi Abu Abdullah al Fasi ameandika vitabu vingi vya thamani kikiwemo kile cha al Mad-khal. Katika kitabu hicho, Ibn Hajj amechunguza masuala mbalimbali yakiwemo ya kiakhlaqi, kifiqi, kijamii na kiuchumi. 

Siku kama ya leo miaka 2045iliyopita, alizaliwa Bi. Mary Ann Evans maarufu kwa jina la George Eliot, mwandishi wa riwaya na simulizi wa Uingereza. Akiwa mtoto mdogo, Evans alipendelea zaidi kusoma vitabu, na taratibu akaingia katika fani ya uandishi. Evans alikuwa na misimamo mikali ya dini ya Kikristo akiwa bado kijana. Hata hivyo misimamo hiyo ilipungua baadaye.

Akiwa na umri wa miaka 30, Ann Evans alifasiri kitabu cha ‘Maisha ya Nabii Issa (as)’ (The Life of Jesus) kilichoandikwa na David Friedrich Strauss. Riwaya za Eliot zinahesabiwa kuwa miongoni wa vitabu maarufu zaidi vya karne ya 19 nchini Uingereza.   

Bi. Mary Ann Evans

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, kufuatia kujiri kwa Vita vya Pili vya Dunia, nchi ya Lebanon ilijipatia uhuru wake.

Lebanon ilitoka katika udhibiti wa utawala wa Othmania mnamo mwaka 1918 Miladia na kudhibitiwa baadaye na Ufaransa. Mwaka 1923 Miladia Ufaransa iliikalia nchi hiyo kwa idhini ya Umoja wa Mataifa. T

angu wakati huo Lebanon ikaanza kushuhudia siasa za ukoloni wa Mfaransa vikiwemo vitendo vya ubaguzi na machafuko. Nchi hiyo ilijipatia uhuru wake mwaka 1943. 

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, John F. Kennedy, rais wa wakati huo wa Marekani aliuawa na raia mmoja wa nchi hiyo akiwa ziarani katika mji wa Dallas huko katika jimbo la Texas.

Kennedy alizaliwa mwaka 1917 na alikuwa mwakilishi wa bunge la Marekani kwa duru tatu kuanzia mwaka 1946 na duru moja alikuwa mwakilishi wa seneti ya nchi hiyo.

Siku kadhaa baadaye Lee Harvey Oswald ambaye alimuua Kennedy naye pia aliuawa na mtu aliyejulikana kwa jina la Jack Ruby na polisi ya Marekani ilidai kuwa mtu huyo vilevile aliaga dunia baadaye akiwa jela kutokana na maradhi ya saratani.

John F. Kennedy

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 242 kuhusu Palestina.

Miongoni mwa vipengee vya azimio hilo ni udharura wa kuondoka askari wa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi zote za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu Juni mwaka 1967 katika vita vya Waarabu na Israel, kusimamishwa operesheni za kijeshi na kutatuliwa kadhia ya wakimbizi wa Palestina kwa njia ya uadilifu.

Hata hivyo kutokana na himaya ya pande zote ya Marekani na nchi za Magharibi kwa utawala ghasibu wa Israel, utawala huo haramu umekataa kutekeleza azimio hilo.     

Katika siku kama hii ya leo miaka 53 iliyopita vikosi vya jeshi la Uingereza viliondoka Ghuba ya Uajemi baada ya kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa takriban karne mbili.

Baada ya kudhoofika sana kwa Uingereza na kuanguka kwa ufalme wake kutokana na Vita vya Pili vya Dunia, pamoja na harakati nyingi za wananchi na kupata uhuru makoloni kadhaa ya Uingereza, mnamo 1968, serikali ya nchi hiyo ilitangaza sera ya kuondoka mashariki mwa Mfereji wa Suez. 

Kulingana na Waingereza, eneo hilo lilijumuisha Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman, Singapore, Malaysia na maeneo mengine kadhaa. 

Hata hivyo, kabla ya kuondoka kwenye Ghuba ya Uajemi, London ilijaribu kuchukua hatua kutimiza malengo yake haramu na kuibua migawanyiko katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuimega na kuitenga Bahrain na Iran.