Ijumaa, tarehe 29 Novemba, 2024
Leo ni Ijumaa tarehe 27 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1446 Hijria sawa na Novemba 29 mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 268 iliyopita, aliaga dunia Abdul Karim bin Ahmad Halabi mpokezi wa hadithi wa Kiislamu.
Alikuwa mashuhuri mno katika upokezi wa hadithi katika zama zake katika mji wa Halab unaopatikana hii leo huko nchini Syria. Halabi alisoma elimu za Fiqh, Usuul al-Fiqh, tafsiri, hadithi na elimu nyingine zilizokuwako katika zama zake kwa baba yake na maulama wengine.
Baadaye Halabi alikuwa kipofu ingawa hata hivyo hakupoteza moyo wa matumaini aliokuwa nao na aliendelea kujihusisha na elimu ya hadithi. Msomi huyo ana vitabu mbalimbali na kimojawapo ni kile kinachoitwa Ad'ayat Safar.
Miaka 81 iliyopita sawa na tarehe 29 Novemba 1943 harakati ya Ukombozi ya kupambana na ufashisti iliundwa nchini Yugoslavia chini ya uongozi wa Marshal Tito.
Wapiganaji wa harakati hiyo walitoa pigo kubwa kwa wanajeshi wa Ujerumani wakati Yugoslavia ilipokuwa ikikaliwa kwa mabavu na jeshi la Ujerumani.
Mwaka 1944 wapiganaji wa harakati ya kupambana na ufashisti nchini Yugoslavia waliwafukuza nchini mwao wanajeshi vamizi wa Ujerumani kwa kusaidiwa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita mwafaka na tarehe 29 Novemba 1947, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha kwa wingi hafifu wa kura suala la kugawanywa ardhi za Palestina baina ya serikali mbili yaani ya Palestina na ya Kiyahudi.
Uamuzi huo usio wa kiadilifu na usio wa kimantiki ulichukuliwa chini ya ushawishi wa serikali za Magharibi hususan Marekani na Uingereza.
Siku ya leo inayosadifiana na tarehe 9 Azar kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsiya huadhimishwa hapa nchini Iran kama siku ya kumbukumbu ya Sheikh Mufid, alimu, msomi na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu.
Jina kamili la mwanazuoni huyu ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Sheikh Mufid, ni Muhammad bin Nu'man na alizaliwa huko Baghdad mwaka 336 Hijria. Alionyesha kipaji kikubwa cha masomo na ufahamu akiwa bado mtoto na ni katika kipindi hicho pia alipoanza kusoma masomo ya Kiislamu.
Sheikh Mufid ameandika vitabu vingi ambavyo vinakadiriwa kufikia 200. Al A'lam, Aamali na Irshad ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya Sheikh Mufid. msomi huyu amezikwa huko Kadhimain nchini Iraq.