Alkhamisi, Disemba 19, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Mfunguo Tisa Jamadithani 1446 Hijria sawa na tarehe 19 Disemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 922 iliyopita, yaani tarehe 17 Jamadithani mwaka 524 Hijiria, alifariki dunia Bari'i Baghdadi, mwanafasihi na malenga mashuhuri wa Kiarabu.
Baghdadi alizaliwa mwaka 443 Hijiria na kuanza kusomea elimu ya nahau na lugha kutoka kwa maulama wakubwa wa kipindi chake. Moja ya athari mashuhuri za Bari'i Baghdadi ni kitabu cha mashairi kilichopewa jina lake.
Malenga na mshairi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81 hali akiwa ni kipofu.

Miaka 859 iliyopita katika siku kama ya leo kulitiwa saini makubaliano ya kisiasa ya Acre katika kipindi cha Vita vya Msalaba baina ya Waislamu na wapiganaji wa Kikristo.
Makubaliano hayo yalitiwa saini kwa ajili ya kukabidhiwa mji wa Acre kwa Wakristo na mkabala wake kuachiliwa huru mateka wa Kiislamu wapatao 3,000. Hata hivyo na bila ya kuheshimu makubaliano hayo, Wakristo waliwaua mateka hao wa Kiislamu suala lililosababisha kuanza tena kwa Vita vya Msalaba ambavyo vilimalizika kwa kushindwa vibaya Wakristo.
Mji wa Acre ulikombolewa na Waislamu katika karne ya 15 Hijiria na ukachukuliwa tena na Wamagharibi mwaka 587.

Katika siku kama ya leo miaka 237 iliyopita mwafaka na tarehe 19 Disemba 1787, nchi ya Kiafrika ya Sierra Leone iliunganishwa na Uingereza baada ya kupita miaka 327 tangu ardhi ya nchi hiyo igunduliwe na wazungu.
Sierra Leone "iligunduliwa" na mtalii wa Uhispania na kukoloniwa. Katika miaka ya kukoloniwa kwake na Uhispania, maelfu ya wanaume na wanawake wa Sierra Leone walichukuliwa watumwa na kwenda kuuzwa katika masoko ya Ulaya. Mwenendo huo uliendelea pia baada ya Waingereza kuishinda Uhispania na kuanza ukoloni wa Uingereza nchini humo.
Mwaka 1961 Sierra Leone ilianza kujitawala na kuwa na utawala unaosimamiwa na jeshi, na mwaka 1971 ikawa na utawala wa Jamhuri.

Katika siku kama ya leo miaka 126 iliyopita alifariki dunia msomi wa Kiislamu, Hajj Mirza Hussain Nuri.
Msomi huyu mkubwa alifikia daraja ya juu katika ibada, ucha-Mungu na ukamilifu wa nafsi. Hajj Mirza Hussein alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, Hadithi, tafsiri ya Qur'ani tukufu na mashairi, na likuwa mwandishi aliyebobea wa vitabu. Vitabu vyake vingi vilihusu elimu za Hadithi, tafsiri na ufafanuzi kuhusiana na maisha ya wasomi wa Kiislamu.
Mirza Hussain Nuri alilipa umuhimu mkubwa suala la kueneza athari za Ahlul-Baiti wa Mtume (saw). Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi, na miongoni mwa athari zake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha "Mustadrakul Wasaail", "Maalimus Sabr", "Jannatul Maawa" na "Nafasur Rahman".
Mirza Hussein Nuri amezikwa katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq.
Miaka 118 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa kiongozi wa Urusi ya zamani, Leonid Brezhnev katika familia maskini nchini Ukraine.
Mwaka 1931, Leonid Brezhnev alijiunga na kuwa mwanachama wa chama hicho cha Kikomonisti. Brezhnev alitwaa uwaziri mkuu wa Russia na uongozi wa Chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani mwaka 1964 wakati Nikita Khrushchev alipokuwa safarini nje ya nchi.
Mashambulizi dhidi ya Czechoslovakia na kukaliwa kijeshi Afghanistan yalifanyika katika zama zake.
Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni Mulla Fat'hullah Gharawi Isfahani aliyejulikana kwa jina la Sheikhu Shari'a Isfahani. Alizaliwa mwaka 1228 Hijria Shamsia huko Isfahan katikati mwa Iran na kupata elimu ya dini katika mji huo. Baadaye kidogo alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had na mwaka 1257 alikwenda Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu na kusoma kwa walimu wakubwa na mashuhuri wa zama hizo.
Ameandika vitabu kadhaa katika masuala ya sheria na fiqhi ya Kiislamu. Sheikhu Shari'a pia alikuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kiutamaduni, kisiasa na kijeshi dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na aliongoza harakati za wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni hao.
Na siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, inayosadifiana na 19 Disemba 1972, kiongozi wa wakati huo wa Uganda, Jenerali Idi Amin Dada, aliwapatia wafanyakazi wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi nchini humo makataa ya siku 12 wakubali kupunguziwa mishahara yao kwa asilimia 40 au waondoke nchini humo.
Zoezi hilo liliwajumuisha karibu wafanyakazi 780 wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi kwenye mashirika mbalimbali nchini Uganda.