Jumapili, 22 Disemba, 2024
Leo ni Jumapili 20 Mfunguo Tisa Jamadithani 1446 Hijria, mwafaka na 22 Disemba 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 2170 iliyopita, duru ya tatu na ya mwisho ya vita vya kihistoria na vya umwagaji damu kati ya tawala za kifalme za Carthage na Roma ilimalizika kwa kupata ushindi Waroma na kuanguka utawala wa Wacartharge. Vita vya falme hizo mbili vilijulikana kwa jina mashuhuri la vita vya Punic. Utawala wa kifalme wa Carthage ulikuwa moja kati ya tamaduni kongwe huko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Mediterrania.

Siku kama ya leo miaka 1454 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Bibi Fatima Zahra, binti mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Bibi Fatima Zahra alilelewa katika nyumba ya wahyi na chini ya malezi bora na mwongozo wa baba yake Mtume Muhammad (saw) na hivyo kuweza kufikia daraja za juu za ukamilifu. Bibi Fatima (as) alikuwa na nafasi kubwa katika kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikimkabili baba yake kutoka kwa washirikina. Mwaka wa pili Hijiria, Bibi Fatima Zahra alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) ambaye ni dhihirisho la haki, uadilifu na uchaji-Mungu katika sherehe ndogo iliyosimamiwa na Mtukufu Mtume Muhammad (saw). Vilevile Bibi Fatima akiwa na Imam Ali alifanikiwa kulea shakhsia adhimu kama Hassan, Hussein na Bibi Zainab (as). Mbali na majukumu ya kulea familia, Bibi Fatima Zahra, alijishughulisha pia na malezi ya jamii.

Miaka 385 iliyopita katika tarehe kama ya leo, alizaliwa Jean Racine malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kifaransa. Racine alianza kazi ya uandishi katika uwanja huo baada ya kusoma kwa muda fulani na kuhitimu akiwa na umri wa miaka 18. Hata hivyo muda fulani baadaye alianza kukosoa kazi hiyo baada ya kuandika mchezo wa tanzia alioupa jina la Andromaque na kupata umashuhuri. Alianza kuakisi matukio ya mfalme wa wakati huo wa Ufaransa. Jean Racine alifariki dunia mwaka 1699 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 331 iliyopita, ulitokea mtetemeko mkubwa wa ardhi katika kisiwa cha Sicily kusini mwa Italia. Kufuatia zilzala hiyo, miji mitatu mikubwa ya kisiwa hicho ilibomolewa na kusababisha hasara kubwa kwa miji mingine yakiwemo makao makuu ya kisiwa hicho yaani Palermo. Mtetemeko huo wa ardhi unahesabiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Italia. Zaidi ya watu 80,000 walipoteza maisha yao katika janga hilo la kimaumbile.

Miaka 126 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alizaliwa huko Khomein Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ruhullah al-Musawi Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul-Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa zaidi za kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha karibu miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, Ufaransa na Uingereza zilihitimisha udhibiti wao wa siku 50 wa bandari ya Port Said nchini Misri na kutoa majeshi yao katika bandari hiyo. Inafaa kuashiria hapa kwamba, baada ya utawala haramu wa Israel kufanya mashambulio katika jangwa la Sinai, mashambulio ya pamoja ya anga ya Uingereza na Ufaransa dhidi ya Misri nayo yalianza. Mashambulio hayo, yalisababisha hasara kubwa katika Mfereji wa Suez. Sababu ya kufanywa mashambulio hayo ambayo baadaye yalikuja kujulikana kama Vita vya Mfereji wa Suez, ni hatua ya Rais Gamal Abdul-Nassir wa Misri ya kutangaza kutaifisha mfereji huo. Umoja wa Mataifa uliiunga mkono Misri wakati wa mashambulio hayo, na kwa utaratibu huo tawala tatu hizo, yaani Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel zikaondoa majeshi yao katika ardhi ya nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita yaani tarehe 22 Disemba mwaka 1989 Miladia, uongozi wa Nicolae Ceausescu, Rais na Mkuu wa chama cha Kikomonisti cha Romania uliangushwa na siku tatu baadaye kiongozi huyo pamoja na mkewe wakanyongwa. Mke wa Ceausescu alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri wa serikali ya Romania. Rais huyo wa zamani wa Romania ya kidikteta aliasisi chama hicho cha Kikomonisti kama walivyofanya watawala wengine wa nchi za Kisoshalisti za Ulaya.
