Dec 24, 2024 02:43 UTC
  • Jumatatu, Disemba 23, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 21 Jamadithani 1446 hijria sawa na Disemba 23 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1062 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Jamaduth-Thani mwaka 384 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya kauli za kihistoria, alifariki dunia Muhsin Bin Ali Tanukhi, mtaalamu wa fasihi, malenga na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu.

Tanukhi alikuwa na kipawa katika uga wa kuhifadhi mashairi na fasihi ambapo ameacha turathi ya mashairi. Aidha kwa muda mfupi Muhsin Bin Ali Tanukhi alikwea hatua za kielimu na kidini katika zama zake na kisha akajishughulisha na kazi ya ukadhi.

Kitabu cha ‘al Faraj Baada sh-Shiddat’ kinachozungumzia matukio ya kihistoria na kijamii ya zama zake, ni miongoni mwa athari zilizoandikwa na msomi huyo. Kitabu kingine cha msomi huyo ni ‘Al-Masaajid’ ambacho kina hekaya na masuala ya akhlaqi na maadili mema. 

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita watu saba miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia walinyongwa, kufuatia hukumu iliyotolewa na mahakama moja ya kimataifa huko Tokyo mji mkuu wa nchi hiyo.

Mahakama hiyo ambayo iliundwa ikiwa ni katika muendelezo wa mahakama ya Nuremberg ya Ujerumani kwa ajili ya kuwahukumu watenda jinai za kivita huko Japan, iliwahukumu viongozi 25 wa Japan ambapo 15 kati yao walihukumiwa kwenda jela. 

Tarehe 23 Disemba miaka 71 iliyopita mkuu wa zamani wa shirika la kuogofya la usalama na la siri la Russia ya zamani ambaye pia alikuwa kiongozi nambari mbili wa nchi hiyo katika zama za Joseph Stalin, Lavrentiy Pavlovich Beria, alihukumiwa kifo na kunyongwa kwa tuhuma za kwenda kinyume na misingi ya sheria za Chama cha Kikomonisti sambamba na kufanya njama dhidi ya serikali.

Katika kipindi cha utawala wa Stalin, Pavlovicha Beria alitoa amri ya kuuliwa watu wengi na akafanya umwagaji damu ndani ya Chama cha Kikomonisti na katika Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani. 

Lavrentiy Pavlovich Beria

Siku kama ya leo, tarehe 23 Disemba mwaka 2013, aliaga dunia Mrussia, Mikhail Kalashnikov ambaye ndiye aliyevumbua bunduki mashuhuri ya Kalashnikov ambayo inajulikana kama AK-47.

Alizaliwa mwaka 1919 katika familia masikini kaskazini mwa Russia, na hakufanikiwa kupata masomo ya juu na hivyo alijiunga na Jeshi la Shirikisho la Sovieti akiwa na umri mdogo. Mwaka 1941, kufuatia shambulizi la Jeshi la Shirikisho la Sovieti dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi, Klashnikov alijeruhiwa na kulazwa hospitalini.

Akiwa hospitalini alitumia muda wa kuuguza majeraha kufanya uchunguzi kuhusu sifa za kipekee za bunduki ya Kimarekani ya M1 Garand na bunduki ya StG 44 ya Ujerumani na kwa kutegemea sifa za silaha hizo mbili akaanza kuunda silaha mpya.

Uundwaji silaha hiyo  ulikamilika mwaka 1947 na kukabidhiwa rasmi Jeshi la Shirikisho la Sovieti mwaka 1951. Bunduki hiyo ilipewa jina la AK-47.   

Mwishoni mwa Umri wake, Klashnikov alikuwa amelazwa hospitalini mjini Moscow kutokana na matatizo ya moyo na Septemba 2013 alihamishwa na kupelekwa katika hospitali moja huko Izhevsk, mji mkuu wa Jamhuri ya Udmurtia katika Shirikisho la Russia na hatimaye 23 Disemba 2013, akiwa na umri wa miaka 94 aliaga dunia akiwa anapata matibabu hospitalini. 

Mikhail Kalashnikov

**