Dec 26, 2024 04:09 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 26 Disemba, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 24 Jumadithani 1446 Hijria sawa na tarehe 26 Disemba 2024.

Siku kama ya leo miaka 902 iliyopita alifariki dunia Ahmad Bin Ali Baihaqi Sabzawari, mmoja wa maulama wakubwa wa elimu ya Qur’ani mjini Nishapur.

Ali Baihaqi Sabzawari, alitabahari katika elimu ya nahaw na lugha kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake, huku akitafsiri aya za Qur’an Tukufu. Aidha alimu huyo alikuwa mahiri katika kisomo cha Qur’an Tukufu.

Ali Baihaqi Sabzawari ameacha vitabu mbalimbali ikiwemo: ‘Taajul-Maswadir’ na ‘al-Muhit Bi’ilmil-Qur’an.’   

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani liliivamia ardhi ya Afghanistan.

Uvamizi huo wa Russia unatambuliwa na kizazi kipya cha viongozi wa nchi hiyo kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa ya ikulu ya Kremlin katika siasa zake za nje. Uvamizi huo wa Urusi ulifanyika kutokana na ombi la Babrak Karmal mmoja wa viongozi wa Afghanistan. Tangu wakati huo Mujahidina wa Afghanistan walianza mapambano dhidi ya jeshi la askari laki moja na 30 elfu la Jeshi Jekundu (Red Army). Katika upande mwingine Marekani ambayo ilitambua kuwepo kwa Urusi ya zamani huko Afghanistan kuwa ni hatari kwa maslahi yake ilianza kuunda makundi ya wapiganaji na kuyasaidia kwa mali na silaha kwa ajili ya kukabiliana na Urusi.

Makumi ya maelfu ya watu waliuawa na wengine kufanywa vilema katika kipindi cha miaka 10 ya uvamizi wa Urusi huko Afghanistan. 

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani, alimu, fakihi mkubwa na mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu ulimwenguni alifariki dunia.

Alizaliwa mjini Golpayegan moja ya miji ya Iran na kusoma masomo ya dini kwa maustadhi stadi na waliokuwa wametabahari kielimu katika zama hizo akiwemo Ayatullah Hairi.

Ayatullah Golpayegani alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum-Iran baada ya kuasisiwa kwake. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika nyuga mbalimbali. 

Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani