Jumamosi, 28 Disemba, 2024
Leo ni Jumamosi 26 Mfunguo Tisa Jamadithani 1446 Hijria mwafaka na 28 Disemba 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita vita vya Dhatus Salasil vilimalizika kwa Waislamu kujipatia ushindi. Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Muhammad (saw), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waende kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea Madina. Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye pia alirejea bila mafanikio. Wakati huo Mtume (saw) alimteua Ali bin Abi Twalib (a.s) kuongoza jeshi la Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (as) aliwashambulia maadui kwa umahiri mkubwa na kurejea Madina na ushindi.

Katika siku kama ya leo miaka 250 iliyopita, Joseph Priestley, mwanakemia na mwanafizikia wa Uingereza alifanikiwa kugundua gesi ya oksijeni. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia. Gesi ya oksijeni ina mchango na nafasi muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu na viumbe vingine hai na huingia katika mwili wa mwanadamu wakati wa kupumua na kuchanganyika na chakula. Matokeo ya kazi hiyo ni kuzalishwa nishati ambayo hutumika katika kubakia hai mwanadamu. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.
Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1895 kwa mara ya kwanza katika historia ya sanaa ya filamu, filamu ya kwanza ya kisa ilioneshwa kwenye mkusanyiko wa watu wengi. Filamu hiyo ilitayarishwa na kuandaliwa na ndugu wawili waliojulikana kwa majina ya Auguste na Louis Lumiere. Miaka iliyofuata ilitengenezwa mitambo bora zaidi ya kurekodi na kuonesha filamu na hatua kwa hatua filamu zenye ubora wa juu na za aina mbalimbali zikaanza kuonyeshwa katika nchi mbalimbali duniani.
Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, katiba ya Iran iliyokuwa imeandikwa na kuandaliwa na Bunge la kwanza la taifa ilitiwa saini na kupasishwa na mfalme wa wakati huo wa Iran Mozaffar ad-Din Shah Qajar. Katiba hiyo ilikuwa na vipengee 51 ambapo baadaye viliongezwa vipengee 107 kama vikamilisho. Katika kipindi cha miaka iliyofuata na katika zama za tawala mbalimbali hususan katika kipindi cha utawala wa kidikteta wa Kipahlavi, katiba hiyo ilifanyiwa marekebisho ya kimsingi. Akthari ya marekebisho hayo yalikuwa ni9 kwa madhara ya mamlaka ya wananchi na Uislamu.
