Dec 29, 2024 03:53 UTC
  • Jumapili, 29 Disemba, 2024

Leo ni Jumapili 27 Mfunguo Tisa Jamadithani 1446 Hijria mwafaka na 29 Disemba 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1055 iliyopita, kwa mujibu wa riwaya mbalimbali aliaga dunia Hussein bin Ahmad Hajjaj mshairi na malenga mashuhuri wa Kishia. Hussein bin Ahmad Hajjaj aliyekuwa malenga mahiri na mwanafsihi mbobezi, aliishi zama moja na Sayyid Murtadha na Sayyid Radhi wanazuoni na wanachuoni wakubwa wa karne ya nne Hijria. Alikuwa mshairi kipenzi wa Ahlul-Baiti (as) na adui mkubwa wa maadui wa dini na ametunga beti nyingi za mashairi katika uwanja huo.  Hussein bin Ahmad Hajjaj aliaga dunia katika eneo lililopo baina ya Baghdad na Kufa na kwa mujibu wa wasia wake, Ibn  Hajjaj alizikwa upande wa chini wa miguu Imam Mussa al-Kadhim (as) katika mji wa Kadhmein Iraq.

Hussein bin Ahmad Hajjaj

 

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Muhammad Ali Shah Qajar aliomba hifadhi katika ubalozi wa Russia mjini Tehran. Kushika kasi na kupanuka wigo wa cheche za Mapinduzi ya Katiba (Constitutional Revolution) katika maeneo mbalimbali ya Iran kulipelekea kuibuka harakati ya kuikomboa Tehran ya wapigania katiba na wakafanikiwa kupata ushindi. ikosi vya Muhammad Ali Shah Qajar vilishindwa jirani na mji wa Tehran. Hatimaye mji wa Tehran ukadhibitiwa na wapigania Katiba. Muhammad Ali Shah Qajar baada ya kuona kuwa amezidiwa nguvu na wanaharakati hao alikimbilia katika ubalozi wa Russia na kuomba hifadhi. Siku hiyo hiyo kukafanyika kikao cha dharura na Muhammad Ali Shah Qajar akauzuliwa na badala yake mwanawe Ahmad Mirza aliyekuwa na miaka 11 akatangazwa kuwa mfalme.

Muhammad Ali Shah Qajar

 

Miaka 94 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Theodor Nöldeke msomi wa Kijerumani na mtaalamu wa mambo ya nchi za mashariki. Alihitimu masomo yake katika taaluma ya teolojia, falsafa pamoja na lugha mbalimbali na kutunukiwa shahada ya uzamivu. Theodor Nöldeke alianza kufundisha Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 25 na kuifanya kazi hiyo kwa miaka mingi. Theodor Nöldeke alikuwa amebobea katika lugha za Kiarabu, KIifarsi, Kituruuki, Kigiriki, Kihispania na Kitaliano.

Theodor Nöldeke

 

Katika siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, mkataba wa kupata uhuru Jamhuri ya Ireland ulitiwa saini baina ya viongozi wa wapigania jamhuri wa Ireland na utawala wa wakati huo wa Uingereza. Hata hivyo kutokana na kuanza Vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Uingereza ilikataa kutekeleza mkataba huo. Baada ya vita hivyo, mnamo mwaka 1949, Jamhuri ya Ireland ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa mkoloni Muingereza. Uhuru wa Ireland ulikuwa matokeo ya mapambano ya karne nane ya wapigania Jamhuri wa Ireland dhidi ya Uingereza.

 

Miaka 46 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, baada ya serikali ya kijeshi chini ya uongozi wa Jenerali Azhari hapa nchini Iran kushindwa kukandamiza vuguvugu la mapinduzi la wananchi Waislamu, Muhammad Reza Shah mfalme wa mwisho wa Iran, alimteuwa Shapour Bakhtiar kuwa Waziri Mkuu. Reza Shah na Marekani walikuwa na matumaini kwamba, Bakhtiar kwa kutumia nara na kaulimbiu zenye mielekeo ya utaifa na siasa ambazo kidhahiri zilikuwa zikionekana kama za kutaka mabadiliko, angeweza kuzuia harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran. Hata hivyo, wananchi wanamapinduzi wa Iran walitambua hila na hadaa hiyo, hivyo walimpinga vikali Bakhtiar na kumuita kuwa kibaraka wa mabeberu. Imam Khomeini (MA) alitoa taarifa na kutangaza kuwa, serikali ya Bakhtiar haikuwa halali na kuwataka wananchi wapambane na serikali hiyo.

 

Tarehe 9 Dei mwaka 1388 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 30 Disemba, yaani miaka 15 iliyopita, mamilioni ya wananchi wa Tehran na miji mingine hapa nchini walifanya maandamano kulalamikia machafuko ya barabarani na himaya ya madola ya Magharibi kwa machafuko hayo. Baada ya uchaguzi wa Rais wa Juni 30, wagombea wawili walioshindwa walilalamikia matokeo ya uchaguzi, lakini hawakuwa tayari kufuatilia malalamiko yao kupitia njia za kisheria. Uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa wagombea hao ulipelekea kutokea machafuko mjini Tehran. Licha ya kuwa machafuko na vurugu za mitaani hazikuwa kubwa lakini ziliathiri amani na utulivu wa wananchi na kuibua tamaa ya Wamagharibi ya kubadilisha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hapa nchini. Maandamano ya mamilioni ya wananchi wa Iran dhidi ya wafanya vujo waliokuwa wakilalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais yalithibitisha kwamba, kinyume na propaganda za maadui, akthari ya wananchi walikuwa wakiyatambua na kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo. Kwa hakika siku ya tarehe 9 Dei (30 Disemba 2009) ilikuwa siku ya kudhihirika uadui na uhasama wa wazi na wa nyuma ya pazia wa maadui wa ndani na nje ya nchi, mkabala wa utawala wa Kiislamu hapa nchini, ambapo maadui wa ndani na nje walilenga shabaha Uislamu, itikadi za kidini, maadili, uongozi wa Iran na mengine mengi ya thamani. Siku hii ya tarehe 9 Dei imepewa jina la "Siku ya Ung'amuzi na Muono wa Mbali".

 

Siku kama ya leo miaka 2 iliyopita, Pele gwiji mashuhuri wa soka aliaga dunia. Edson Arantes do Nascimento anayejulikana kama Pele, alizaliwa mnamo Oktoba 23, 1940 huko Tinejos, Brazil. Pele ambaye anajulikana kama mmoja wa wachezaji bora wa soka katika historia, alikulia katika familia maskini na alikuwa akipenda sana mpira wa miguu tangu utoto. Pele alianza kucheza soka akiwa na umri wa miaka 10 na alijiunga na timu ya Santos akiwa na umri wa miaka 15. Aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya soka ya Brazil kwa mara ya kwanza akkiwa na umrii wa miaka 17. Alishiriki kombe la dunia mara nne akiwa na timu ya soka ya Brazil. Aidha pele alichezea Brazil mechi 92 na kurfunga mabao 77. Mwaka 2000 Pewle alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa karne. Pele a;ishinda mataji 3 ya kombe la dunia akiiwa na timu ya soka ya Brazil katika miaka ya 1958, 1962 na 1970.

Edson Arantes do Nascimento anayejulikana kama Pele