Jan 04, 2025 03:03 UTC
  • Ijumaa, Januari 3, 2025

Leo ni Ijumaa Pili Rajab 1446 Hijria sawa na Januari 3 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 1225 iliyopita, kulingana na kalenda ya Hijria,  alizaliwa Ibn Rumi, malenga mashuhuri wa Kiarabu mjini Baghdad, Iraq.

Alianza kusoma elimu ya awali kwa baba yake akiwa kijana mdogo, na baadaye akasoma kwa walimu wakubwa wa enzi zake. Aidha alipata kujifunza elimu za zama zake kama vile fasihi na mashairi.

Ibn Rumi alikuwa akisoma sana mashairi ya kumsifu Imam Hassan Askari, mmoja wa Ahlubaiti wa Mtume (saw) kutokana na mapenzi yake makubwa aliyokuwanayo kwa watu wa familia ya Mtume wa Allah (as). Malenga huyo alifariki dunia mwaka 283 Hijiria. 

Ibn Rumi

Katika siku kama ya leo miaka 1006  iliyopita, alifariki dunia Abu Raihan Biruni msomi, mnajimu na mwanahisabati mkubwa wa Kiirani huko katika mji wa Ghazne katikati mwa Afghnaistan ya sasa.

Abu Raihan Biruni alikuwa hodari katika elimu za historia, jiografia na hisabati, tiba na utengenezaji wa dawa. Akiwa safarini nchini India, msomi huyo wa Kiirani alikutana na kufanya mijadala na maulama na watawala wa zama hizo. Abu Raihan alikusanya taarifa muhimu alizokuwa akizihitaji kwa ajili ya kuandika kitabu chake alichokiita 'Tahqiq Ma Lilhind' baada ya kujifunza lugha ya Sanskriti yaani lugha ya Kihindi ya kale.

Katika kitabu hicho, Abu Raihan ameandika taarifa muhimu kuhusu sayansi, itikadi, mila na desturi za Wahindi. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingine vingi kuhusu elimu ya nujumu, mantiki na falsafa.

Abu Raihan Biruni

Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, inayosadifiana na Januari 3, 1993 kulitiwa saini makubaliano ya Start-2 kati ya Marais wa zamani wa Russia na Marekani, Boris Yeltsin na Bill Clinton. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi hizo mbili zinapaswa kupunguza theluthi mbili za silaha zao za nyuklia. Makubaliano ya Start-1 yenye lengo hilohilo yalitiwa saini mwaka 1987 kati ya Marais Mikhael Gorbachev wa Russia na Ronald Reagan wa Marekani. Hata hivyo badala ya kuanza kuharibu silaha zake za nyuklia, Marekani ilijilimbikizia sialaha zaidi za aina hiyo suala ambalo liliilazimisha pia Russia kusitisha mpango wa kuanza kuharibu silaha zake za atomiki.

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo kulifanyika mkutano wa Guadeloupe kati ya viongozi wa serikali za Marekani, Uingereza, Ujerumani ya Magharibi na Ufaransa kwa ajili ya kuchunguza masuala kadhaa muhimu ya kimataifa hususan Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Mkutano huo ulifanyika katika kisiwa cha Guadeloupe kilichoko magharibi mwa Bahari ya Atlantic ambacho ni koloni la Ufaransa.

Katika mkutano huo uliofanyika siku 41 kabla ya ushindi kamili wa harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran washiriki wote walikiri kwamba, Mfalme wa wakati huo wa Iran, Shah Pahlavi, ataondolewa madarakani isipokuwa Jimmy Carter rais wa wakati huo wa Marekani ndiye pekee aliyekuwa na matumaini ya kubakia madarakani utawala wa Shah kwa msaada wa jeshi.

Hata hivyo mkutano huo wa Guadeloupe haukuwa na mbinu ya kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi wa Iran na uliishia kukiri nguvu kubwa ya mapinduzi hayo na mustakbali wake mwema.   

Tarehe 14 Dei miaka 46 iliyopita wakati wa kilele cha harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah, Jenerali Robert E. Huyser aliyekuwa mshauri mkuu wa kijeshi na Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga la Marekani aliwasili kwa siri mjini Tehran. Jenerali Huyser alikuwa na jukumu maalumu la kuisaidia serikali ya Marekani katika kuchukua maamuzi ya baadaye na kupata habari za ndani za Iran katika kipindi cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.

Katika kipindi chote cha zaidi ya siku 30 za kuwepo kwake mjini Tehran Jenerali Huyser alikutana mara moja tu na Shah na katika kikao hicho iliainishwa saa na siku ya kuondoka Shah nchini Iran.

Jenerali Robert E. Huyser