Jumapili, 05 Januari, 2025
Leo ni Jumapili 4 Rajab 1446 Hijria mwafaka na 5 Januari 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1422 iliyopita vilianza vita vya miaka 24 kati ya falme za Iran na Roma. Vita hivyo viliibuka kufuatia kuuawa Maurice, aliyekuwa mfalme wa Roma na ambaye pia alikuwa muungaji mkono na rafiki wa karibu wa Mfalme Khosrow Parviz wa Iran. Kufuatia mauaji hayo ya Maurice, mtoto wake alikuja Iran na kumuomba msaada Mfalme Khosrow. Mfalme huyo wa Iran na kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Maurince, alituma jeshi lililojizatiti kwa silaha kwenda kuishambulia Roma ambapo kwa kipindi kifupi liliweza kuteka miji mingi ya nchi hiyo. Baada ya ushindi huo, mfalme mpya wa Roma alimtuma mjumbe wake kuja Iran kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya amani na mfalme wa Iran, hata hivyo Mfalme Khosrow Parviz ambaye alikuwa tayari ameingiwa na kiburi cha kupata ushindi mkubwa katika vita hivyo, alikataa mpango wa amani na hivyo akawa ameendeleza vita hivyo. Vita hivyo ambapo pande mbili zilipata ushindi katika vipindi tofauti, viliendelea kwa muda wa miaka 24.

Miaka 854 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, alifariki dunia malenga wa Kiislamu, Muhammad ibn Ali al-Wasiti maarufu kwa jina la Ibn Muallim. Alizaliwa mwaka 501 Hijiria. Mashairi ya malenga huyo yalibeba ujumbe wa maadili na tabia njema na masuala mengine ya kijamii kwa kutumia lugha nyepesi. Baadhi ya mashairi ya Ibn Muallim yanahusiana na masuala ya kiroho na kiirfani. Athari pekee ya Ibn Muallim ni kitabu cha tungo za mashairi ya malenga huyo.
Siku kama ya leo miaka 334 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1691, ilichapishwa na kusambazwa noti ya kwanza huko Ulaya. Noti hiyo ilichapishwa na Benki ya Stockholm na kutumiwa kama fedha. Kabla ya kuchapishwa noti hiyo nchini Sweden, miamala ya kibiashara ilikuwa ikifanyika kwa kutumia sarafu za dhahabu zenye pembe nne. Moja kati ya noti za awali kabisa kuchapishwa nchini Sweden, inahifadhiwa kwenye makumbusho ya Benki ya Stockholm.

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita alifariki dunia Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi na kutokuwa na wizani. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh". ***
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita kulitokea hamasa ya mashahidi wa Huweize iliyoongozwa na Shahidi Alamul Huda katika miezi ya mwanzoni mwa uvamizi wa Iraq dhidi ya ardhi ya Iran. Mwezi Dei mwaka 1359 Hijria Shamsia na baada ya jeshi la Iran ya Kiislamu kuvishinda vikosi zaidi ya viwili vya jeshi la Iraq huko kusini mwa eneo la Susangerd, kundi moja la Jeshi la Sepah la Ahwaz huko kusini mwa Iran lilitumwa katika mji wa Huweize kwenda kuulinda mji huo mbele ya mashambulizi ya Iraq. Hata hivyo kutokana na kuchelewa kufika zana na hujuma kubwa ya Iraq, jeshi la Iran lililazimika kurudi nyuma. Wakati huo zaidi ya wapiganaji mia moja wa Jeshi la Sepah, wapiganaji wa kujitolea na wanafunzi wa vyuo vikuu wafuasi waaminifu wa Imam Khomeini wakiongozwa na Sayyid Muhammad Hussein Alamul Huda walibakia katika mji huo wa Huweize wakipambana na adui na wakauawa shahidi. Baadaye jeshi la Iraq liliuvunja kabisa mji wa Huweize na kuusawazisha na ardhi. Pamoja na hayo ushujaa wa vijana hao shupavu wa Iran waliosabilia roho zao kulinda ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu umebakia hai katika historia ya Iran.