Jan 06, 2025 03:01 UTC
  • Jumatatu, tarehe 06 Januari, 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 5 Rajab 1446 Hijria sawa na Januari 06 mwaka 2025.

Tarehe 5 Rajab miaka 1202 iliyopita aliuawa shahidi Abu Yusuf Yaqub ibn Is'haq, maarufu kwa jina la Ibn Sikkit, msomi wa Kiislamu na mtaalamu mkubwa wa lugha ya Kiarabu.

Alizaliwa katika mji wa Khuzestan unaopatikana kusini magharibi mwa Iran. Ibn Sikkit alielekea mjini Baghdad na familia yake na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo.

Umaarufu wa Ibn Sikkit katika elimu ulimfanya Mutawakkil, mmoja kati ya watawala wa Abbasia kumwalika kwa lengo la kuwafundisha watoto wake. Ibn Sikkit alikuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW); jambo hilo lilimkasirisha sana Mutawakkil na alichukua hatua ya kumuua. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni kile kiitwacho "Islahul Mantik." 

Siku kama ya leo 164 iliyopita ilianzishwa nchi ya Romania. Mpango wa kuasisiwa nchi ya Romania ulibuniwa tarehe 13 Disemba 1859 kwa kuunganishwa miji miwili midogo ya Moldavia na Wallachia.

Miaka miwili baadaye majimbo na miji mingine ilijiunga na umoja huo na kuundwa nchi ya Romania. 

Miaka 89 iliyopita katika siku kama hii ya leo, wanawake wa Kiirani walipigwa marufuku kuvaa vazi la Kiislamu la aina yoyote kufuatia amri ya Rezakhan Pahlavi.

Rezakhan alitoa amri hiyo baada ya kutekelezwa mpango wa kubadili mavazi ya wanaume nchini Iran. Mpango huo ulitekelezwa kwa lengo la kufuta thamani za Kiislamu na badala yake kuiga utamaduni wa Kimagharibi.

Ridhakhan alitekeleza mpango huo wa kupiga marufuku vazi la hijabu kwa wanawake wa Kiislamu nchini Iran baada ya safari yake nchini Uturuki na kufuata nyayo za Kemal Atatürk Rais wa wakati huo wa Uturuki aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi ambaye aliwapiga marufuku wanawake wa nchi hiyo kuvaa mavazi ya Kiislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, Gholamreza Takhti mchezaji na bingwa wa mchezo wa mieleka wa Kiirani aliuawa kwa njama zilizopangwa na utawala wa wakati huo wa Shah.

Takhti Alizaliwa mjini Tehran katika familia iliyokuwa na maisha ya kati na kati. Gholamreza Takhti alijulikana mno kwa tabia yake ya huruma, ukweli na mapenzi yake kwa watu.  Katika kipindi cha uhai wake na wakati wa kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa, Gholamreza Takhti alifanikiwa kuipatia Iran medali 9 za dhahabu na fedha katika mashindano ya Olimpiki.

Takhti ni miongoni mwa wachezaji wa Kiirani waliotwaa medali nyingi za dhahabu na fedha katika mashindano muhimu ya kimataifa.

Gholamreza Takhti

Miaka 47 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakilalamikia kuchapishwa makala iliyomvunjia heshima mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Maandamano hayo yalizidisha vuguvugu na kasi za Mapinduzi ya Kiislamu kuelekea katika ushindi.

Utawala wa Shah ambao ulikuwa ukifahamu vyema ushawishi na uungaji mkono mkubwa wa Imam Khomeini miongoni mwa wananchi, ulikuwa ukidhani kwamba kumvunjia heshima Imam Khomeini kungeweza kupunguza kiwango cha mapenzi na uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa shakhsia huyo.

Katika kufanikisha lengo hilo, gazeti la Ittilaat lililokuwa likitolewa mjini Tehran liliandika makala ya kumvunjia heshima Imam Khomeini katika toleo lake la mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya. Hata hivyo makala hiyo ilikuwa kama cheche ya moto iliyochochea zaidi harakati za mapinduzi na hatimaye tarehe 22 mwezi Bahman mwaka 1357, utawala kibaraka wa Shah ukang'olewa madarakani kwa mapambano ya wananchi wa Iran.