Jan 07, 2025 02:40 UTC
  • Jumanne, Januari 7, 2025

Leo ni Jumanne tarehe 6 Rajab 1445 Hijria sawa na Januari 7 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 963 iliyopita Hassan Sabbah mmoja wa viongozi wakubwa wa Waislamu wa Shia Ismailiya, alitwaa udhibiti wa ngome muhimu na imara ya Alamut, iliyo karibu na mji wa Qazvin, kaskazini mwa Iran.

Hassan Sabbah ambaye kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya hapo alikuwa akiwalingania watu kumfuata yeye, aliimarisha utawala wake baada ya kutwaa udhibiti wa ngome hiyo na muda mfupi baadaye alidhibiti miji mingine.

Baada ya kudhibiti ngome hiyo ya Alamut, kuliongezeka tabligh (linganio) za kuwataka watu wajiunge na madhehebu ya Shia Ismailiya na wafuasi wa wake walifanya mauaji dhidi ya viongozi wa utawala wa Seljuqi, akiwemo Khoja Nidham al-Mulk. Ngome ya Alamut iliendelea kuwa tegemeo la wafuasi wa Ismailiya nchini Iran hadi pale ilipoangukia mikononi mwa utawala wa Hulagu Khan mwaka 654 Hijiria. Hassan Sabbah alifariki dunia mwaka 518 Hijiria.

Tarehe 6 Rajab miaka 930 iliyopita, alifariki dunia Abu Muhammad Qasim bin Ali Basri maarufu kwa jina la Ibn Hariri, mwanafasihi na mwandishi mashuhuri wa Kiirani aliyekuwa akiishi Basra nchini Iraq.

Ibn Hariri ndiye mwandishi wa kitabu maarufu cha 'Maqamaat' ambacho ni cha aina yake katika taaluma ya fasihi ya Kiarabu. Katika kitabu hicho, Ibn Hariri alieleza siri za fasihi ya lugha ya Kiarabu katika kalibu ya hikaya na semi nyepesi za hekima.   

Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Tabatabai, mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu na maulamaa wapigania uhuru wa Iran.

Wakati wa mapinduzi ya kikatiba nchini Iran, Sayyid Muhammad Tabatabai alikuwa akihesabika kuwa mmoja kati ya viongozi wakubwa wa mapinduzi hayo. Tabatabai alishirikiana na Sayyid Abdullah Behbahani ambaye naye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya kikatiba dhidi ya utawala wa Qajari nchini Iran. 

Ayatullah Sayyid Muhammad Tabatabai

Miaka 82 iliyopita yaani mnamo tarehe 7 mwezi Januari mwaka 1943 aliaga dunia Nikola Tesla mwanafikia mzaliwa waYugoslavia.

Nikola alizaliwa mwaka 1857 na alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza masomo ya fizikia wakati akiwa shuleni. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa.

Umeme mbadala au Altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux).

Nikola Tesla

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, majeshi ya Vietnam yaliishambulia Cambodia na kupelekea dikteta wa nchi hiyo Pol Pot kuikimbia nchi hiyo na hatamu za uongozi kuchukuliwa na Heng Samrin.

Pol Pot alikuwa kiongozi wa kundi la Khmer Rouge la Cambodia lililokuwa likifuata fikra za Kimao. Katika kipindi cha chini ya miaka mitatu cha uongozi wake nchini Cambodia, Pol Pot akishirikiana na kundi la Khmer Rouge aliwauwa watu kati ya milioni 1.5 na milioni 2. 

Pol Pot

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Suleiman Khater mmoja wa polisi wa mpakani katika jangwa la Sinai, alikufa shahidi akiwa jela.

Akionyesha upinzani wake dhidi ya mkataba wa Camp David, Oktoba mwaka 1985 aliwaangamiza Wazayuni kadhaa katika jangwa la Sinai. Serikali ya Misri baada ya kumtia mbaroni askari huyo, ilimhukumu kifungo cha maisha jela.

Hata hivyo baada ya muda kiwiliwili cha Suleiman Khater kilipatikana katika kituo cha matibabu cha magereza kikiwa kimening'inia na serikali ya Misri ilidai kwamba, mfungwa huyo alijiuwa.

Suleiman Khater

Na Tarehe 18 Dei mwaka 1385 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 18 iliyopita alifariki dunia mhakiki na mwanahistoria wa Iran Hujjatul Islam Ali Dawwani. Msomi huyu alizaliwa mwaka 1308 Hijria Shamsia karibu na mji wa Kazerun ulioko kusini mwa Iran.

Alielekea Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kupata elimu za Kiislamu akiwa na umri wa miaka 14 na kurejea nchini miaka mitano baadaye. Ali Dawwani aliendelea kutafuta elimu katika mji mtakatifu wa Qum na kusoma kwa wanazuoni wakubwa kama Imam Ruhullah Khomeini na Ayatullah Borujerdi hadi alipopata daraja ya ijtihadi. Alibobea sana katika elimu ya historia na ameandika vitabu vingi katika uwanja huo.

Miongoni mwa vitabu vyake ni "Fakhari za Uislamu", "Mbora wa Wanawake Duniani" na "Harakati ya Wanazuoni wa Iran". 

Ali Dawwani