Jan 12, 2025 02:38 UTC
  • Jumapili, 12 Januari, 2025

Leo ni Jumapili 11 Rajab 1446 Hijria ambayo inasadiifiana na 12 Januari 2025 Miladia.

Miaka 1175 iliyopita mwafaka na leo, alizaliwa mjini Baghdad mtaalamu wa fasihi, lugha na mfasiri wa Qur'ani Tukufu, Abubakar Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn al Anbari. Alijifunza elimu ya Hadithi baada ya kukamilisha masomo yake ya lugha na sayansi za Qur'ani tukufu. Ibn al Anbari alikuwa na uwezo wa hali ya juu wa kuhifadhi na kushika vitu kichwani mwake. Alikuwa mtu mwema na mchamungu na mbali na kujishughulisha na kufundisha na kulea vizazi vya maulamaa, mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya "Adabul Kaatib" na "Dhamaairul Qur'ani." Alifariki dunia mwaka 328 Hijiria akiwa na umri wa miaka 57.

Ibn Anbari

 

Miaka 875 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mjini Damascus, Syria mwanahistoria mkubwa na mtaalamu wa Hadithi Ibn Asakir. Alisoma elimu za Qur'ani, hadithi, fiq'hi na usulu fiq'hi kwa wasomi wakubwa wa mjini Damascus. Baada ya hapo Ibn Asakir alianza safari ndefu yenye lengo la kukamilisha masomo yake na kupata elimu katika vituo vya kielimu vya Baghdad, Kufa, Mosul, Neishabur, Marv, Isfahan na Hamedan. Msomi huyo ameandika vitabu 134 kikiwemo kile cha "Tarikh Dimishqi."

Ibn Asakir

 

Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, alizaliwa Jack London mwandishi mashuhuri wa nchini Marekani. Kwa miaka kadhaa Jack alifanya safari katika eneo la ncha ya Kaskazini na maeneo mengine na kupata bahati ya kufahamiana na koo na kaumu mbalimbali katika maeneo hayo sambamba na kubainisha taswira ya masuala hayo katika vitabu vyake.  Jack London aliishi kwa muda wa miaka 40 huku akijihusisha na kazi ya uandishi kwa muda wa miaka 18. 

Jack London

 

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita mapigano makali kati ya polisi wa utawala wa Shah na wananchi wa Iran yalitokea wakati yalipofanyika maandamano makubwa ya wananchi katika miji kadhaa ya Iran. Wananchi wengi wanamapambano waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika maandamano hayo. Katika siku hiyo pia wanachuo na wakazi wa mji wa Tehran ambao walikuwa wamekusanyika kwa wingi mbele ya Chuo Kikuu cha Tehran walitangaza upinzani wao dhidi ya utawala wa Shah na wakitaka kurejea Tehran Imam Khomeini (ra), kutoka uhamishoni huko Paris nchini Ufaransa. ***  

Kushika kasi maandamano dhidi ya utawala wa Shah

 

Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, shambulio la kwanza la kemikali la jeshi la utawala wa wakati huo wa Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam lilitekelezwa dhidi ya Iran ikiwa ni chini ya miezi minne tu tangu Iraq ianzishe vita vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Shambulio hilo la kinyama ambalo lilitekelezwa kilomita 50 magharibi mwa mji wa Ilam magharibi mwa Iran, lilipelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa. Jeshi la utawala wa Baath, likipata himaya na misaada ya madola ya Magharibi na Umoja wa Kisovieti, lilitumia mara chungu nzima silaha zilizopigwa marafuku dhidi ya raia na wapiganaji wa Iran katikakipindi chote cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya taifa hili. Takribani watu elfu kumi waliuawa shahidi na laki moja na elfu 30 walijeruhiwa kufuatia mashambuluio hayo ya silaha zilizopigwa marufuku. ***

Jinai ya utawala wa Saddam iliyotokana na kutumia silaha hatari za kemikali dhidi yay Iran