Jan 13, 2025 03:35 UTC
  • Jumatatu, 13 Januari, 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 12 Rajab 1446 Hijria sawa na tarehe 13 Januari 2025.

Siku kama ya leo miaka 1414 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Abbas bin Abdul Muttalib, ami yake Bwana Mtume (saw) na mmoja wa shakhsia wakubwa wa Kikuraishi.

Alijulikana kwa tabia njema, mwenendo mzuri, busara na maarifa ya hali ya juu. Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba, Abbas bin Abdul Muttalib aliukubali Uislamu kwa siri kabla ya Bwana Mtume kuhamia Madina na alikuwa akimpelekea Mtume habari za harakati za washirikina mjini Makka.

Mwaka wa 8 Hijria Abbas bin Abdul Muttalib aliungana na Waislamu na baada ya Fat'hu Makka aliteuliwa na Bwana Mtume kuchukua jukumu la kutoa huduma ya maji kwa watu wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba. 

Katika siku kama hii ya leo miaka  1240 iliyopita aliaga dunia Abu Hudhayfah, mpokezi wa Hadith, habari za kihistoria na visa vya Mitume.

Aliishi kwa muda katika miji ya Makka na Madina na akajishughulisha na kujifunza Hadith.

Abu Hudhayfah alikuwa mpokezi wa kutegemewa wa Hadith. Moja ya vitabu vyake muhimu ni "Al-Mubtada", ambacho kinahusu kuumbwa kwa mwanadamu na visa vya manabii. Kazi nyingine muhimu ya Abu Hudhayfah ni maelezo ya riwaya ya Imam Ja'far al-Sadiq (AS) kuhusu safari ya Mi'raji ya Mtume Muhammad (SAW). 

Tarehe 13 Januari miaka 575 iliyopita alizaliwa baharia na mvumbuzi wa Kireno, Bartholomew Diaz.

Baada ya kusafiri katika Bahari ya Atlantic kuelekea kusini mwaka 1488, Diaz alidai kuwa amegundua Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) katika sehemu ya kusini zaidi ya bara la Afrika.

Miaka kumi baadaye baharia mwenzake, Vasco Da Gama, naye pia alifanikiwa kugundua njia ya baharini kuelekea India kupitia eneo hilo.

Bartholomew Diaz

Siku kama ya leo miaka 334 iliyopita aliaga dunia George Fox mwanamageuzi wa Kikristo wa nchini Uingereza.

Fox alizaliwa 1624 katika familia ya kidini. George Fox alishindwa kustahamili mgongano uliokuwako katika maneno na vitendo vya makasisi na wafuasi wa Ukristo na vilevile vita vya watawala wa zama hizo.

Akiwa na umri wa miaka 19, Fox alikata shauri kufanya utafiti kwa ajili ya kutafuta ukweli. George Fox alikuwa akiamini kwamba, kuna ulazima wa kurejea katika mafundisho asili ya Ukristo na kujiepusha na umwagaji damu na wakati huo huo kusimama kidete kukabiliana na dhulma. Hata hivyo, Fox nae pia alitumbukia katika makosa kwenye itikadi zake. Pamoja na hayo, fikra zake zilipingana na mafundisho ya Ukristo katika zama hizo.

Mara kadhaa George Fox alitiwa mbaroni na kutupwa jela na mamia ya wafuasi wake walikuwa wakiteswa gerezani. Harakati yake ya kupigania mabadiliko ya kidini iliendelea baada ya kuaga kwake dunia na harakati hiyo ingalipo. 

George Fox

Miaka 84 iliyopita katika siku kama hii mkutano wa kihistoria wa nchi waitifaki za Ulaya katika Vita vya Pili vya Dunia ulifanyika mjini London, Uingereza.

Mkutano huo ulifanyika kufuatia pendekezo la Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza Winston Churchill, lengo kuu lilikuwa kuratibu siasa za wakuu wa nchi za Ulaya katika medani za vita dhidi ya nchi mbili za Ujerumani na Italia.

Vilevile nchi za Uingereza, Uholanzi, Ubelgiji, Ufaransa, Ugiriki, Norway, Luxembourg na Denmark zilishiriki katika mkutano huo. ***