Jan 14, 2025 03:25 UTC
  • Jumanne, tarehe 14 Januari, 2025

Leo ni Jumanne tarehe 13 Rajab 1446 Hijria sawa na Januari 14 mwaka 2025.

Leo tarehe 13 Rajab zinaanza siku zinazojulikana katika dini kuwa ni "Siku Nyeupe" au siku za ibada ya Itikafu ambazo ni siku za tarehe 13, 14 na 15 za mwezi huu wa Rajab.

Katika siku hizi waumini wanashauriwa kufanya ibada ya itikafu ya kukaa na kubaki katika sehemu au mahali maalumu hususan misikitini na maeneo matakatifu kwa ajili ya ibada na kumdhukuru Mwenyezi Mungu SW. Watu wanaofanya itikafu hutakiwa kufunga Saumu siku tatu mfululizo wakiwa katika jitihada za kuondoka katika minyororo ya dunia hii finyu na kujikuribisha kwa Allah.

Ibada ya itikafu imehimizwa sana na Mtume Muhammad (saw) na maimamu watoharifu katika kizazi chake. 

Siku kama ya leo miaka 1469 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba, Ali bin Abi Twalib AS, ambaye ni binamu, mkwe na Khalifa wa Mtume Muhammad (saw). Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib.

Katika kipindi chake cha utotoni, Ali bin Abi Talib alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu SAW, na alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu. Mwishoni mwa mwaka wa Pili Hijria, Imam Ali AS alimuoa Bibi Fatimatul Zahra binti ya Mtume Mtukufu SAW.

Imam Ali AS alishiriki kwenye vita vyote bega kwa bega na Mtume Mtukufu SAW isipokuwa vita vya Tabuk, na alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini Imam Ali bin Abi Talib alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge.   

Haram ya Imam Ali (as) huko Nafaj nchini Iraq

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita ulianza mkutano wa Casablanca nchini Morroco. Mkutano huo uliofanyika wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na rais wa zamani wa Marekani Franklin Delano Roosevelt na Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill kama viongozi wa nchi mbili kuu za waitifaki na kujadili mpango wa kushambulia Sicily nchini Italia na nchi za washirika. 

Mwishoni mwa mkutano huo wawakilishi wa nchi zilizoshiriki walitoa taarifa ya pamoja ambayo kwa mujibu wake nchi waitifaki ziliapa kuendeleza vita hadi wakati wa kusalimu amri mahasimu wao bila ya masharti.   

Mkutano wa Casablanca

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Dey 1357 Hijria Shamsia, kulitokea mapigano makubwa baina ya jeshi la utawala wa Shah na wananchi wa Iran kufuatia maandamano ya mara kwa mara ya wananchi dhidi utawala huo wa kidikteta.

Katika mapigano hayo baadhi ya wanajeshi waliotambua sababu za mapambano ya wananchi, waliamua kuzikimbia kambi zao za kijeshi na kujiunga katika safu za wananchi. Kujiunga wanajeshi na safu za wananchi ilikuwa bishara njema ya mabadiliko makubwa katika moyo na muundo wa jeshi la utawala wa Shah.

Wakati huo huo Imam Khomeini ambaye alikuwa uhamishoni nchini Ufaransa, alikuwa akituma taarifa mara kwa mara akiwahimiza wanajeshi kujiunga na mapambano ya wananchi, kuuhami na kuutetea Uislamu na sheria zake na kuwafukuza wageni waliokuwa wakidhibiti kila kitu nchini Iran. 

Wanajeshi wakijiunga na wananchi

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita maafisa wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walitekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya Salah Khalaf maarufu kwa jila la Abu Iyad akiwa pamoja na maafisa wengine wawili wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia.

Salah Khalaf alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu na kiongozi nambari mbili wa Fat'h baad ya Yaser Arafat. 

Mauaji ya viongozi hao wa ngazi za juu wa PLO tena baada ya kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi nyingine yaani Tunisia, yalionyesha kwamba utawala haramu wa Israel hauheshimu sheria yoyote ile katika suala la kuwaangamiza wapinzani wake.     

Abu Iyad akiwa pamoja na Arafat

Siku kama ya leo miaka 14 iliopita, sawa na tarehe 14 Januari 2011 Rais Zainul Abidin Bin Ali wa Tunisia na dikteta wa nchi hiyo alikimbilia Saudi Arabia kufuatia vuguvugu la mapinduzi ya wananchi.

Kukimbia nchi Zainul Abidin, kulihitimisha utawala wa kiimla uliodumu kwa nusu karne wa Habib Bourquiba pamoja na Zainul Abidin Bin Ali na wananchi wa Tunisia wakaonja ladha ya uhuru. Zainul Abidin aliingia madarakani mwaka 1987 kupitia mapinduzi ya kijeshi bila umwagaji damu na kumwondoa madarakani Habib Bourguiba aliyekuwa amejitangaza kuwa rais wa maisha wa nchi hiyo. Bin Ali aliiongoza Tunisia kwa mkono wa chuma kwa miaka 23 huku akiendeleza siasa za kutegemea Wamagharibi na kupiga vita Uislamu.

Kujichoma moto kijana mmoja muuza mboga katika kulalamikia dhulma na ukatili wa maafisa usalama wa utawala wa nchi hiyo, kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kiufisadi wa Bin Ali na hatimaye kupinduliwa dikteta huyo.

Zainul Abidin Bin Ali