Jumatano, 15 Januari, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 14 ya mwezi Rajab 1446 Hijria mwafaka na tarehe 15 Januari 2025.
Siku kama ya leo miaka 1444 iliyopita yaani tarehe 14 Rajab mwaka wa pili Hijiria, kulijiri vita vya kwanza baina ya Waislamu na washirikiana wa Makka mwanzoni kabisa mwa kudhihiri dini Tukufu ya Kiislamu.
Mapigano hayo ya kwanza ya Waislamu baada ya kusimamisha dola mjini Madina, yaliongozwa na Abdullah bin Jahsh Asadi, huku upande wa pili ukiongozwa na Omar bin al Hadhrami ambaye alikuwa kiongozi wa msafara wa Maquraish. Katika mapigano hayo Omar bin al Hadhrami aliuawa. Mapigano hayo yanajulikana katika historia ya Kiislamu kwa jina la Sariyyatu Abdullah bin Jahsh.

Miaka 230 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Aleksandr Griboyedov mwandishi na mwanasiasa asiye na ustahiki wa Urusi.
Alikuwa na umahiri mkubwa katika uandishi wa drama na michezo ya kuchekesha. Aleksandr Griboyedov hakupata mafanikio ya uga wa siasa. Wakati wa kujiri vita vya pili vya Iran na Urusi alikuwa miongoni mwa maafisa wa Kirusi. Baada ya Iran kushindwa katika vita hivyo, Griboyedov alipewa amri na mtawala wa Tsar mwaka 1828 aje Tehran ili akawachukue mateka wa Kirusi waliokuwa wakishikiliwa Iran.
Majigambo na kutokuwa na tajiriba pamoja na utumiaji mabavu wake wakati wa safari yake hii, ni mambo yaliyochochea hisia za wananchi wa Iran na kuanzisha uasi dhidi yake ambao ulipelekea kuuawa kwake mwaka 1829.
Katika siku kama ya leo miaka 186 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Januari 1839, nchi ya El Salvador ilijitangazia rasmi uhuru wake baada ya kusambaratika Muungano wa Amerika ya Kati, amma nchi hiyo haikupata amani na utulivu hata baada ya kupita karne moja.
El Salvador ambayo ilikuwa ikikoloniwa na Uhispania kwa miaka kadhaa, ilijipatia uhuru wake mwaka 1821, na ulipofika mwaka 1824 ilijiunga na Muungano wa Amerika ya Kati, na hatimaye uliposambaratika muungano huo, nchi hiyo ilijitegemea kikamilifu. El Salvador ilikabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi mwaka 1931, baada ya kuporomoka bei ya kahawa katika soko la dunia, zao lililokuwa likitegemewa nchini humo.
Hali mbaya ya kiuchumi iliwakasirisha wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kuanza kuibuka uasi wa wananchi na wanachuo dhidi ya dikteta Jenerali Maximiliano Hernandez Martinez wa El Salvador.

Tarehe 26 Dey 1357 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi, mfalme wa mwisho wa Iran alitoroka nchini kwa kisingizio cha kwenda kupata matibabu nje ya nchi, baada ya kushadidi wimbi la harakati za Mapinduzi.
Muhammad Reza Pahlavi alichukua kiti cha ufalme mwaka 1320 Hijria Shamsia baada ya serikali ya Uingereza kumpeleka uhamishoni baba yake, Reza Shah, kwa sababu aliiunga mkono Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Siku chache kabla ya tukio hilo, Imam Ruhullah Khomeini ambaye wakati huo alikuwa Ufaransa, alitoa ujumbe mzito akisema kuwa: "Safari ya Shah bila ya kung’oka madarakani haitabadilisha lolote na utawala wa kifalme nchini Iran unapaswa kuangushwa kikamilifu."

Tarehe 15 Januari miaka 24 iliyopita ensaiklopidia ya Wikipedia ilianza kazi katika mtandao wa intaneti.
Lengo la kuanzishwa ensaiklopidia hiyo limetajwa kuwa ni kupanua maarifa na uelewa wa watu kupitia njia ya kushirikishwa watu wote katika mradi huo. Insaiklopidia hiyo kubwa ya intaneti ina taarifa na makala kuhusu mamilioni ya vitu kwa lugha mbalimbali na ndiyo inayotembelewa zaidi na watu katika mtandao huo.
Hata hivyo uwezekano wa kila mtu kuingia na kuandika atakavyo katika ensaiklopidia hiyo umeshusha chini hadhi na nafasi yake ya kielimu. Zaidi ni kwamba licha ya kuwa wasimamizi wa Wikipedia wanadai hawapendelei upande wowote lakini kwa kawaida makala zinazohusiana kwa njia moja au nyingine na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel huwa za upendeleo.
Kituo kikuu cha Wikipedia kiko katika jimbo la Florida nchini Marekani na ensaiklopidia hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za Marekani.
