Jumamosi, 18 Januari, 2025
Leo ni Jumamosi 17 Rajab 1446 Hijria mwafaka na 18 Januari 2025.
Siku kama ya leo miaka 336 iliyopita alizaliwa mwandishi na mwanafalsafa maarufu wa Ufaransa, Charles de Montesquieu. Alikuwa miongoni mwa wasomi ambao fikra na itikadi zao zilikuwa na taathira kubwa katika harakati ya mapinduzi ya Ufaransa na alikuwa mtu wa kwanza kutoa nadharia ya udharura wa kutenganishwa nguvu kuu tatu za dola. Kitabu maarufu zaidi cha Charles de Montesquieu ni "The Spirit of the Laws" (Roho ya Sheria) ambacho kilichapishwa mwaka 1748 huko Geneva. Katika kitabu hicho alichunguza aina mbalimbali za serikali zilizojitokeza katika kipindi chote cha historia, ada na sheria za kimaumbile, sheria za kibinadamu na uhusiano baina yao. Kitabu kingine cha mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni "Persian Letters" (Barua za Kiiran). Alifariki dunia mwaka 1755. ***
Miaka 325 iliyopita katika siku kama ya leo tarehe 17 Rajab mwaka 1121 Hijria, alifariki dunAi Allamah Fadhil Sheikh Sulaiman Bahrani, aliyekuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu. Sheikh Abul-Hassan Sulaiman Ibn Abdillah Ibn Ali Ibn Hassan Bahrani Mahuzi, maarufu kwa jina la Muhaqqiq Bahrani, mmoja wa maulama wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia mwanzoni mwa karne ya 12 Hijiria, alizaliwa katikati ya mwezi wa Ramadhani mwaka 1076 Hijiria. Alibobea katika elimu ya Hadithi, wapokezi wa Hadithi, historia na maisha ya mtukufu Mtume (saw) na Ahlu Baiti wake (as). Sheikh Abdullah Samahiji na Sayyid Hashim Bahrani, mwandishi wa tafsiri ya Qur'ani ya Al-Burhan na Sheikh Ahmad Bahrani, ni miongoni mwa wanafunzi wa Allamah Fadhil Sheikh Sulaiman Bahrani. ***
Tarehe 18 Januari miaka 110 iliyopita 'Mkataba wa Siri' ulitiwa saini kati ya nchi tatu za Ufaransa, Uingereza na Russia wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Lengo kuu la mtakaba huo lilikuwa ni suala la kujiunga utawala wa Kiothmani (Ottoman Empire) na waitifaki wa Vita vya Kwanza vya Dunia, yaani Ujerumani na Austria. Kwani kujiunga utawala huo na waitifaki kungekata uhusiano wa jeshi la majini la Russia na waitifaki wake katika Bahari Nyeusi. Baada ya kutiwa saini mkataba huo, nchi waitifaki zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya lango bahari la Dardanelles linalounganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Mediterranean.

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita yaani tarehe 18 Januari 1919, ulifanyika mkutano wa kihistoria wa amani wa Versailles baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa kuwashirikisha wawakilishi wa nchi 27 kutoka mabara matano duniani. Mkuu wa mkutano huo alikuwa Georges Clémenceau, waziri mkuu wa wakati huo wa Ufaransa. Nchi tano zilizokuwa zimeshindwa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia yaani Ujerumani, Austria, Hungary, Bulgaria na dola la Othmania, hazikushiriki kwenye mkutano huo. Kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini katika mkutano huo, Ujerumani ililazimishwa kulipa fidia kubwa na kutoa sehemu za ardhi zake kwa Austria. Mkutano huo ulikuwa utangulizi wa kuanzishwa Jumuiya ya Kimataifa.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran wenye imani na umoja walifanya maandamano makubwa kupinga mabaki yaliyosalia ya utawala wa kifalme Shah, yaani serikali ya Shapur Bakhtiyar. Waandamanaji hao walitaka serikali hiyo ya kifalme itangazwe kuwa si halali, na pia kung'olewa utawala wa Shah na badala yale kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Siku hiyo Imam Khomeini MA akiwa mjini Paris alitoa ujumbe wa maandishi kwa wananchi wa Iran akisema kama tunavyonukuu: "Kwa uwezo wake Mola hivi karibuni nitaungana nanyi ili niweze kuwatumikia na kushirikiana bega kwa bega na matabaka yote ya wananchi kuelekea katika njia ya kujitawala na kuwa huru Iran." Mwisho wa kunukuu. ****
Na siku ya leo tarehe 29 Dei inajulikana nchini Iran kwa anwani ya "Siku Taifa ya Gaza". Siku hii ni kumbukumbu ya kumalizika vita vya siku 22 vya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza ambapo vita hivyo vilifikia tamati kwa ushindi wa muqawama na mapambano ya Kiislamu huko Gaza. Kutokana na vyombo vya Magharibi kuficha jinai za utawala haramu wa Israel na kwa upande mwingine kutokana na hamasa kubwa iliyooonyeshwa na wananchi madhulumu wa Gaza katika kutetea ardhi zao, siku hii imepewa jina la "Siku ya Kitaifa ya Gaza. ***
