Jumatatu, 20 Januari, 2025
Leo ni Jumatatu tarehe 19 Rajab 1446 Hijria mwafaka na tarehe 20 Januari 2025.
Siku kama ya leo miaka 1437 vilitokea vita vya Tabuk baina ya Waislamu na jeshi la Roma. Vita vya Tabuk ni miongoni mwa vita vya mwisho vya Mtume Muhammad (saw).
Sababu ya kutokea vita hivyo ni kwamba, msafara wa kibiashara wa Sham ulimtaarifu Mtume (saw) kwamba mfalme wa Roma ametayarisha jeshi na kulituma Madina. Kwa msingi huo Mtume Muhammad (saw) aliwaanuru Waislamu kujitayarisha kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la mfalme wa Roma.
Waislamu wengi walijitayarisha kwa ajili ya vita hivyo licha ya masafa marefu, msimu wa joto kali, mashaka ya safari hiyo ngumu na kuwadia msimu wa mavuno. Hatimaye jeshi na wapiganaji elfu 30 la Waislamu liliwasili eneo la vita lakini halikukuta jeshi la mfalme wa Roma eneo hilo.
Japokuwa hakukutokea mapigano wakati huo, lakini tukio hilo lilidhihirisha nguvu ya Waislamu, utayarifu wao wa kukabiliana na majeshi vamizi na moyo wao wa kujitolea kwa ajili ya Allah.
Vita hivyo vya Tabuk pia vinajulikana kwa jina la "al Fadhiha" kwa maana ya mfedheheshaji kutokana na kwamba, vililifedhehesha kundi la wanafiki waliokataa kujiunga na msafara huo kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la Roma.

Miaka 973 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 19 Rajab mwaka 474 Hijria Qamaria Abul Walid Sulaiman bin Khalaf Maliki, faqihi maarufu wa karne ya Tano Hijria Qamaria aliaga dunia huko Andalusia ambayo leo inajulikana kama Uhispania.
Alikuwa hafidh na mfasiri wa Qur'ani Tukufu mbali na kubobea katika fasihi na mashairi. Abul Walid awali alifunza Fiqhi na taaluma ya Hadithi za Mtume SAW huko Andalusia na kisha akaendelea kufundisha huko Makka na Baghdad.
Baadhi ya vitabu mwanazuoni huyo ni, "Tafsirul Qur'an", "An-Nasikh Walmansukh" na Al-Isharah."

Miaka 125 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia John Ruskin mwandishi, mwanafalsafa na mkosoaji mashuhuri wa Uingereza.
Msomi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Ruskin alizaliwa mwaka 1819 mjini London. Awali Ruskin alifunzwa na wazazi wake akiwa nyumbani kabla ya kujiunga na chuo cha mjini London na akiwa huko akaanza kutunga mashairi.
Malenga huyo wa Uingereza alikuwa mkosoaji wa sekta ya sanaa na alibainisha mitazamo yake kuhusu sanaa katika kitabu chake alichokipa jina la "modern painters".

Tarehe 20 Januari miaka 105 iliyopita alizaliwa mtengeneza filamu mashuhuri wa Italia, Federico Fellini. Alikuwa mtayarishaji filamu mwenye mbinu makhsusi.
Fellini alianza kuandika rasimu ya filamu (scenario) mwaka 1938 na baadaye akaingia katika uwanja wa kutayarisha filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia Fellini alishirikiana na mtengenezaji filamu mwingine wa Italia, Roberto Rossellini, katika utengenezaji wa filamu ya "Rome, Open City" (Roma, Mji Usiokuwa na Ulinzi).
Miezi sita kabla ya kufariki dunia, Federico Fellini alitunukiwa tuzo ya fahari ya Oscar kutokana na kazi zake kubwa katika medani ya filamu. Filamu mashuhuri zaidi za Fellini ni "Saa Mbili Unusu", "Juliet of the Spirits" na "The Sweet Life".

Siku kama ya leo miaka 46 liyopita sambamba na kuanza kutetereka nguzo za utawala wa Shah nchini Iran mkabala wa wimbi kubwa la mashinikizo ya wananchi na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu, serikali ililazimika kuwaachia huru wafungwa waliokuwa katika jela za Shah na wananchi Waislamu wa Iran wakawapokea watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa miaka mingi katika jela hizo.
Alasiri ya siku hiyo maafisa wa Jeshi la Anga la Iran walifanya maandamano na kutangaza uungaji mkono wao kwa harakati ya taifa la Kiislamu la Iran. Siku hiyo hiyo pia magazeti ya Iran yaliandika habari iliyokuwa na kichwa kilichokolezwa wino kwamba: "Imam Khomeini Kurejea Iran Siku Kadhaa Zijazo".
Habari hiyo ilizusha wimbi la hamasa na furaha kubwa kati ya wananchi wanamapinduzi wa Iran na kila mtu alianza kujitayarisha kwa ajili ya kwenda kumpokea kiongozi wa kihistoria wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini.

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, mamluki wa utawala wa kidikteta wa Shah nchini Iran walishambulia Chuo Kikuu na Tehran na na kuwajeruhi wanafunzi wengi.
Wanachuo hao walikuwa wakiandamana kudai haki za wanafunzi waliokuwa wameandamana na kisha kukabiliwa na vitendo vya kikatili vya maafisa usalama. Askari hao waliwapiga vibaya makumi ya wanachuo na wahadhiri na kuharibu nyenzo za masomo kama vitabu na maabara.
Baada ya tukio hilo, serikali ya wakati huo kwa kuhofia kuenea malalamiko ilikifunga Chuo Kikuu cha Tehran kkwa muda wa miezi miwili na nusu.
