Ijumaa, tarehe 24 Januari, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 23 Rajab 1446 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 24 Januari 2025.
Siku kama ya leo miaka 358 iliyopita, mkataba wa Breda ulitiwa saini kati ya Uingereza na Uholanzi.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Uholanzi ambayo haikuwa na uwezo wa kulinda makoloni yake katika bara lililokuwa ndio kwanza limegunduliwa la Amerika, iliyakabidhi makoaloni yake hayo kwa Uingereza.
Eneo muhimu ambalo Uingereza ilikabidhiwa ni New York, ambalo leo kijiografia linapatikana mashariki mwa Marekani.

Katika siku kama ya leo miaka 166 iliyopita, kisima cha kwanza kabisa cha mafuta katika historia kilichimbwa huko Pennsylvania nchini Marekani.
Kisima hicho kilichimbwa na Edwin Laurentine Drake kikiwa na kina cha urefu wa mita 230. Uchimbaji wa kisima hicho uliendelea kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Vifaa vilivyotumika kuchimbia kisima hicho vimehifadhiwa hadi leo katika jumba moja la makumbusho nchini Marekani.

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Winston Churchill, mwanasiasa maarufu wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 91.
Churchill alizaliwa mwaka 1874 na mwaka 1895 alijiunga na jeshi la Uingereza na kushiriki katika vita vya kikoloni.
Mwaka 1900 Winston Churchil aliingia katika Bunge la Uingereza akikiwakilisha chama cha Kihafidhina na mara kadhaa aliongoza wizara mbalimbali na kwa vipindi viwili alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.
Tarehe 5 Bahman miaka 46 iliyopita matabaka mbalimbali ya wananchi wa Iran waliendeleza maandamano makubwa katika miji mbalimbali dhidi ya utawala kibaraka wa Shah licha ya mamluki wa mfalme huyo kutumia mbinu zote za ukatili na ukandamizaji.
Siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran walipuuza marufuku iliyokuwa imetangazwa ya kuzuia mikusanyiko ya zaidi ya watu mawili katika miji mbalimbali ya Iran.
Ukandamizaji mkubwa wa maajenti wa utawala wa Shah ulipelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya raia. Siku hiyo hiyo idadi kubwa ya maafisa wa Jeshi la Anga la Iran ilijiunga na harakati ya mapambano ya wananchi katika mitaa ya jiji la Tehran na kufanya maandamano dhidi ya utawala wa Shah.
Askari hao walitangaza utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini na harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu.
