Jan 25, 2025 03:02 UTC
  • Jumamosi, 25 Januari, 2025

Leo ni Jumamosi 24 Rajab 1446 Hijria mwafaka na 25 Januari 2025

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita, ngome ya Khaibar ambayo ilikuwa moja ya ngome madhubuti na imara zaidi za Mayahudi ilitekwa na kudhibitiwa na Imam Ali (as), mkwewe Mtume Mtukufu (saw). 

Mayahudi ambao hawakuacha kueneza uadui wao wa jadi dhidi ya Uislamu walikuwa wakiendeshea njama zao huko Khaibar kaskazini mwa mji mtakatifu wa Madina, ambako walikuwa wamejenga ngome saba muhimu, ambazo waliamini kuwa hazingepenyeka wala kudhibitiwa na adui. 

Katika mwaka wa saba Hijiria Mtume (saw) alibashiri kutekwa kwa mji wa Khaibar. Muda si mrefu na baada ya kuvunja mzingiro uliokuwa umewekwa na maadui, jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kudhibiti ngome kadhaa kati ya hizo saba isipokuwa mbili. Hatimaye Mtume aliwahutubu makamanda wa jeshi hilo kwa kusema: 'Kesho nitampa bendera mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda pia, na Mwenyezi Mungu ataiteka ngome hii kupitia mikono yake.

Siku iliyofuata, Mtume alimpa Imam Ali (as) uongozi wa jeshi ambapo alipigana vita vya kishujaa na hivyo kuweza kudhibiti ngome ya mwisho ya Mayahudi huko Khaibar.

Ngome ya Khaybar katika mji wa Madina

Katika siku kama ya leo miaka 1107 iliyopita, Abu Nasr Muhammad Farabi, Mwanafalsafa, mwanahesabati na msomi mashuhuri wa Iran aliaga dunia. 

Alizaliwa mwaka 259 Hijiria katika mji wa Farab ilioko kusini mwa nchi ya Kazakhstan  ya leo. Baada ya kupata masomo ya msingi katika mji huo, Farabi aliamua kwenda mjini Baghdad huko Iraq ili kuendeleza masomo yake na hasa ya mantiki na falsafa. Werevu mkubwa aliokuwanao ulimuwezesha kusoma masomo mengi ya zama zake lakini alizingatia zaidi somo la falsafa. 

Mwanafalsafa huyo  mashuhuri aliyefahamika zaidi kwa majina ya  Muallim ath-Thani, Ustadh wa Falsafa na Malik al-Hukamaa alifanya juhudi kubwa za kuunganisha fikra za wanafalsafa tofauti na hasa za Aristotle na Platon, akiamini kulikuwa na falsafa moja tu.

Picha ya kulia ni mahali lilipo kaburi la Abu Nasr Muhammad Farabi katika mjnhi wa Damascus Syria

Katika siku kama ya leo miaka 569 iliyopita, kazi ya uchapishaji vitabu ilianza na kitabu cha kwanza kabisa kikachapishwa kwa kutumia mashine iliyogunduliwa na Mjerumani, Johannes Gutenberg. 

Mashine hiyo ya uchapishaji ilikuwa hatua muhimu katika njia ya uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.' 

Hii leo kurasa kadhaa zilizobakia za kitabu hicho zinahifadhiwa katika majumba ya makumbusho. 

Miaka 234 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Allamah Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Ulum, mtaalamu wa elimu ya irfan na msomi mkubwa wa Kiislamu. 

Alizaliwa mwaka 1155 Hijiria katika mji mtukufu wa Karbala, Iraq na kusoma elimu za dini ya Kiislamu katika mji huo kwa baba yake mzazi ambaye alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa zama hizo na kwa wasomi wengine. Akiwa kijana, Allamah Bahrul-Ulum alifanikiwa kukwea daraja za juu za elimu na kufikia ijtihadi, na baada ya hapo akaelekea Najaf. 

Msomi huyo alijishughulisha na kazi mbalimbali za kijamii na alipendwa sana na watu. Sayyid Bahrul-Ulum aliiishi miaka saba mjini Mash’had, Iran na miaka miwili huko Hijaz, Saudi Arabiia ambapo pia aliendelea kujishughulisha na kazi za kielimu kiasi cha kumfanya imam wa Msikiti wa Makkah wakati huo, kujiunga na madh’habu ya Shia. 

Vitabu vya ‘Al-Maswaabih’ ‘Mishkaatul-Hidaayah’ ‘Fawaaidulr-Rijaaliyah’ na diwani ya mashairi ni miongoni mwa athari za msomi huyo. 

Allamah Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Ulum

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita vijidudu maradhi vinavyosababisha maradhi ya ukoma viligunduliwa na tabibu na mhakiki wa Ujerumani kwa jina la Gerhard Henrik Armauer Hansen. 

Ugonjwa huo huambatana na vidonda vikali vinavyovuruga na kuharibu maumbo ya muathirika. Vijidudu maradhi vya ugonjwa huo wa ukoma pia hukusanyika katika mishipa ya neva na kusababisha uharibifu katika sehemu kubwa ya mishipa hiyo. Maradhi hayo hujitokeza zaidi katika maeneo yenye joto. 

Licha ya maendeleo makubwa ya kisayansi yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa wa ukoma, lakini njia ya kutibu maradhi hayo sugu bado haijapatikana na idadi kubwa ya waathirika wake wanaendelea kuteseka katika nchi mbalimbali duniani. 

Gerhard Henrik Armauer Hansen

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, kilianza kipindi cha Uwaziri Mkuu wa Amir-Abbas Hoveyda aliyekuwa mmoja kati ya watu waliokuwa watiifu kwa utawala wa kifalme wa Shah hapa Iran. 

Baada ya kunyongwa Hassanali Mansour, Waziri Mkuu wa wakati huo wa utawala wa Shah, Amir-Abbas Hoveyda  aliyekuwa Waziri wa Hazina katika Baraza la Mawaziri la Mansour aliamriwa kuunda serikali akiwa Waziri Mkuu. Amir-Abbas Hoveyda alishikilia wadhifa huo kwa takribani miaka 13 hadi mwaka 1977. ***

Amir-Abbas Hoveyda

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, kundi lililokuwa dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu lililojulikana kwa jina la Muungano wa Wakomonisti, lilishambulia mji wa Amol wa kaskazini mwa Iran. 

Kundi hilo lilikuwa likijidanganya kwamba, eneo hilo litakuwa kituo chao cha mashambulio yao ya baadaye kaskazini mwa Iran. Vikosi vya wapiganaji na wananchi wanamapinduzi wa mji huo kwa muda mfupi walifanikiwa kuzima mashambulio ya kundi hilo lililokuwa dhidi ya mapinduzi.

Kusimama kidete  mtaa kwa mtaa wananchi wa mji wa Amol dhidi ya mashambulio ya kundi hilo kumeufanya mji wa Amol utambulike na kuwa mashuhuri kwa jina la mji wa ngome elfu moja. 

Siku  kama ya leo miaka 18 iliyopita Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mara ya kwanza kwa harakati hiyo kushiriki kwenye zoezi hilo. 

Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na waangalizi wa kigeni, Hamas ilifanikiwa kupata viti 76 kati ya jumla viti 132 vya Bunge la Palestina licha ya propaganda chafu zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo Hamas ilimuarifisha Ismail Hania kama Waziri Mkuu na kutangaza kwamba itaunda serikali ya umoja wa kitaifa. 

Hata hivyo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na muitifaki wake Israel, zilikataa kutambua rasmi serikali hiyo iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Palestina.