Jan 26, 2025 02:26 UTC
  • Jumapili, 26 Januari, 2025

Leo ni Jumapili 25 Rajab 1446 Hijria ambayo inasadiofiana na 26 Jnauari 2025 MIladia.

Siku kama ya leo miaka 1263 iliyopita, Imam Musa Kadhim (as) mmoja wa wajukuu watoharifu wa Mtume Mtukufu (saw) aliuawa shahidi. Imam Kadhim (as) alizaliwa mwaka 128 Hijiria huko katika eneo la Ab'waa lililoko baina ya miji mitakatifu ya Madina na Makka. Mtukufu huyo kwa miaka 20 alipata malezi na elimu muhimu kutoka kwa baba yake ambaye ni Imam Jaafar as-Swadiq (as). Baada ya kuuawa baba yake huyo, Imam Kadhim (as) alipata fursa ya kuuongoza Umma wa Kiislamu kwa muda wa miaka 35, ambapo alipata mateso na mashaka mengi katika njia hiyo. Katika zama zake ambazo zilisadifiana na ustawi mkubwa wa utamaduni na elimu ya Kiislamu pamoja na kuimarishwa uhusiano na mataifa ya kigeni, Imam alifanya juhudi kubwa za kueneza mafunzo ya Kiislamu katika mataifa hayo kupitia wanafunzi wake. Mbali na hayo, Imam pia aliendesha mapambano makali dhidi ya watawala dhalimu wa Bani Abbas. Hatimaye Haroun ar-Rashid kutoka ukoo wa Bani Abbas aliyehofia sana kuporomoka kwa utawala wake, alimfunga jela Imam Kadhim (as). Licha ya kufungwa jela lakini Imam (as) hakusimamisha shughuli zake za kulingania dini na na mafundisho sahihi ya Uislamu. Hatimaye Haroun Rashid alifanya njama ya kumuua Imam kwa kumpa sumu. Huku tukitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kuuawa shahidi Imam Kadhim (as), tunakunukulieni hapa moja ya semi zake zenye mafunzo na busara kubwa. Imam anasema: 'Njia bora zaidi ya kumkurubia Mwenyezi Mungu baada ya kumjua ni kusimamisha swala, kuwatendea wema wazazi wawili na kuachana na husuda na majivuno.' 

 

Miaka 202 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Edward Jenner tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (small pox). Jenner alizaliwa mwaka 1749. Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Kuanzia hapo ugonjwa huo wa ndui ulitibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. mwaka 1979 maradhi hayo yalitokomezwa kabisa duniani. *** 

Edward Jenner

 

Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita mfumo wa Jamhuri ulitangazwa nchini India na siku hii ikapewa jina la Siku ya Kitaifa ya India. Baada ya India kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza Jawaharlal Nehru alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu huku Rajendra Prasad akichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa mfumo wa India, wadhifa wa urais ni wa kiheshima tu na Waziri Mkuu ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali. India ina jamii ya karibu watu bilioni moja na milioni hamsini na ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa zaidi duniani baada ya China. ***

 

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, nchini Iran kulifanyika maandamano makubwa ya mamilioni ya watu baada ya kuundwa serikali ya muda ya mapinduzi. Maandamano hayo yalifanyika kuunga mkono uamuzi huo wa Imamu Khomeini. Katika siku hii wananchi wa Iran katika miji mbalimbali walitokeza na kukusanyika mabararani na kupaza sauti kwa pamoja wakitaka kuondolewa madarakani serikali ya Bakhtiyar.

Maandamano dhidi ya Shah

 

Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Abdul Aziz Tabatabai Yazdi. Alizaliwa mwaka 1348 Hijria katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq na kupata elimu kwa wanazuoni wakubwa wa mji huo akiwemo Atayullah Sayyid Abdul Aala Musawi Sabzavari, Sheikh Sadra Badkubeh na Sayyid Abul Qassim al Khui. Alielekea katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran mwaka 1354 Hijria Shamsia na kujishughulisha na kazi za uandishi na uhakiki. Alkuwa miongoni mwa wataalamu mashuhuri na wakubwa wa historia, hadithi, rijali na amefanya kazi kubwa ya kutayarisha faharasa ya Maktaba Kuu ya Haram ya Imam Ridhaa (as) katika mji mtakatifu wa Mahs'had na Maktaba ya Amirul Muuminin katika mji wa Najaf. Ayatullah Abdul Aziz Tabatabai Yazdi ameandika makumi ya vitabu vikiwemo vya Adhwaa A'ala al Dhari'a na al Mahdi fii al Sunna Annabawiyyah. 

Ayatullah Sayyid Abdul Aziz Tabatabai Yazdi.

 

Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani, Bi Annemarie Schimmel. Bibi Schimmel alipendelea mno kutalii na kupata maarifa kuhusu ustaarabu wa Kiislamu na alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin akiwa na umri wa miaka 19. Prf. Annemarie Schimmel alifundisha kwa miaka mingi historia ya dini na irfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani na Uturuki. Mbali na kujua lugha za Kijerumani na Kiingereza, Bi Schimmel alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kiurdu, Kibengali na Kituruki kwa ajili ya kupata maarifa zaidi kuhusu masuala ya Kiislamu. Prf. Annemmarie Schimmel ameandika vitabu kadhaa kuhusu masuala ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kile cha "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Mwanamke katika Irfani ya Kiislamu".

 Annemarie Schimmel