Jumatatu, tarehe 27 Januari, 2025
Leo ni Jumatatu tarehe 26 Rajab 1446 Hijria sawa na Januari 27 mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 1449 iliyopita, Abu Twalib ami ya Mtume Muhammad (SAW) na baba wa Imam Ali (A.S) alifariki dunia wakati Waislamu walipokuwa chini ya mzingiro wa washirikina wa Makka.
Abu Twalib alikuwa pamoja na Waislamu wengine huko katika Shiibi Abi Twalib. Mtume Muhammad (SAW) alikuwa chini ya uangalizi wa Abu Twalib tangu alipokuwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake, Abdul Muttalib. Abu Twalib alisilimu baada ya kubaathiwa Mtume na alikuwa muungaji mkono na mtetezi mkubwa wa Mtume Mtukufu dhidi ya washirikina wa Kiquraishi.
Kabla ya kuaga dunia, Abu Twalib aliwausia jamaa na marafiki zake kufuata Uislamu na kumtetea Mtume Muhammad (saw).
Miaka 134 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Ilya Ehrenburg mwandishi wa Umoja wa Kisovieti yaani Urusi ya zamani.
Ilya alifanya kazi ya uandishi habari kwa miaka kadhaa huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na utunzi wa mashairi pia. Ehrenburg alifahamika vyema nchini humo kama mwandishi wa hadithi na mwanahabari, khususan pale alipokuwa akiripoti matukio katika Vita vya Kwanza vya Dunia, vya Pili na vile vya ndani vya Uhispania.
Mwandishi huyo wa Kirusi aliandika vitabu visivyopungua 100 vikiwemo vya "Tufani" na "Kuanguka Paris". Ilya alifariki dunia mwaka 1967.
Katika siku kama ya leo miaka 125 iliyopita mfamasia wa Kijerumani Felix Hoffmann alitengeneza dawa ya kwanza ya kutuliza maumivu.
Dawa hiyo hii leo inajulikana kwa jina la Aspirin. Waingereza pia waliamua kutengeneza dawa hiyo katika kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia baada ya uingizaji dawa hiyo nchini Uingereza kusimamishwa.
Mbali na kutuliza maumivu, Aspirin ina sifa nyingine kadhaa ambazo ni pamoja na kuzuia damu isigande na kuzuia mshtuko wa moyo. ***
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini yalitiwa saini mjini Paris, Ufaransa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa kipindi cha miaka minne.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Paris, Marekani ilikubali kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini. Japokuwa baada ya kutiwa saini makubaliano hayo vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini havikusitishwa, lakini serikali ya Washington ililazimika kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini baada ya kupata hasara kubwa za hali na mali.
Makubaliano ya Paris yalikuwa pigo kubwa kwa siasa za uingiliaji kati na za kibeberu za Marekani nchini Vietnam ambazo zilianza kutekelezwa mwaka 1964.
Miaka 46 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kundi kubwa la wanazuoni wa Kiislamu lilianzisha mgomo wa kuketi katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran baada ya Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah, Shapoor Bakhtiyar, kumzuia Imam Khomeini kurejea nchini Iran akitokea uhamishoni.
Wanazuoni hao walisema, sharti pekee la kusitisha mgomo huo ni kuruhusiwa Imam Khomeini kurejea nchini.
Mgomo huo ulikuwa miongoni mwa matukio muhimu katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kwani kwa upande mmoja, serikali ya wakati huo ya Shah iliyokuwa ikiungwa mkono na Marekani, ilifanya jitihada kubwa za kumzuia Imam Khomeini asirejee nchini, na kwa upande mwingine ilikuwa ikifanya njama za kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi kwa kutoa ahadi na kutumia vitisho.
Mgomo huo wa wanazuoni wa Kiislamu uliowashirikisha maulamaa mashuhuri kama Shahid Ayatullah Murtadha Mutahhari na Ayatullah Muhammad Beheshti, ulikifanya Chuo Kikuu cha Tehran kuwa kituo kikuu cha harakati za mapambano.

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliendeleza utafiti wake wa masuala ya anga za mbali kwa kutuma kiumbe hai angani ikitumia roketi.
Kiumbe huyo hai alikuwa tumbili ambaye alirejea ardhini salama katika utafiti huo.
Majaribio hayo yaliyokuwa na mafanikio yaliwaonesha walimwengu mafanikio na maendeleo ya masuala ya anga ya Iran katika kipindi hicho cha vikwazo vizito vya kidhalimu vya Marekani na waitifaki wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
