Jan 28, 2025 02:54 UTC
  • Jumanne, tarehe 28 Januari, 2025

Leo ni Jumanne 27 ya mwezi Rajab 1446 Hijria mwafaka na 28 Januari 2025.

Siku kama ya leo miaka 1459 iliyopita, Mtume Mtukufu Muhammad Mustafa (s.a.w) alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu.

Kipindi hicho Mtume Muhammad (s.a.w) alikuwa na umri wa miaka 40. Mtume Muhammad (saw) alianza kutafakari na kudurusu maumbile ya dunia akiwa bado mdogo na daima alikuwa akifirikia njia za kunyanyua juu utukufu wa mwanadamu.

Alikuwa maarufu kwa ukweli, uaminifu na kutenda mema. Jumla ya sifa hizo njema zilimfanya Muhammad (s.a.w) kuwa shakhsia mwenye hadhi na heshima kubwa katika jamii. Alipitisha muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa. Malaika Jibrail alimteremkia Muhammad akiwa katika pango hilo na kumpa bishara ya kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake kwa walimwengu wote.

Tangu siku hiyo Mtukufu huyo alipewa jukumu kubwa la kuongoza wanadamu na kupambana na ujahili, ukafiri, dhulma na uonevu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu.   

Pango la Hiraa

Siku kama ya leo miaka 979 iliyopita alizaliwa faqihi, mfasiri wa Qur'ani na msomi wa Kiislamu na Kiirani, Jarullah Zamakhshari. Mwanazuoni huyu pia alikuwa gwiji katika elimu za hadithi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Muqaddimatul Adab na Asasul Balagha. Kitabu muhimu zaidi cha Jarullah Zamakhshari ni tafsiri ya Qur'ani ya al "Kash'shaf".   

Mahali lilipo kaburi la Zamakhshari

Katika siku kama ya leo miaka 218 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashiful-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kiislamu.

Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashiful-Ghitaa alianza kufundisha na kufanikiwa kulea wanafunzi wengi na vilevile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.   

Sheikh Ja'afar Kashiful-Ghitaa

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita inayosadifiana na tarehe 27 Rajab 1415 Hijria, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kurusha hewani matangazo yake kwa mara ya kwanza.

Matangazo ya Radio Tehran yalianza kurushwa kwa muda wa nusu saa tu nyakati za usiku, na yalifunguliwa kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kubaathiwa na kupewa Utume, Bwana wetu Muhammad (SAW). 

Lengo la kuasisiwa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kufikisha sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wanaodhulumiwa wa bara la Afrika, kuelimisha na kufichua njama za ubeberu wa kimataifa dhidi ya bara hilo. 

Siku hii ya leo ya tarehe 28 mwezi Januari, inaadhimishwa kote duniani kama Siku ya Kimataifa ya Kuwasaidia Wagonjwa Wenye Maradhi ya Ukoma.

Siku hii ilipewa jina hilo na Raul Follivero, raia wa Ufaransa yapata nusu karne iliyopita. Wakati huo dunia ilikuwa na watu milioni 15 waliokuwa wakisumbuliwa na maradhi hayo. Kufuatia hali hiyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliiainisha tarehe 28 Januari kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukoma.

Tangu yalipoanza mapambano dhidi ya ukoma waathirika wa maradhi hayo wamepungua na kufikia watu milioni mbili. Hata hivyo licha ya juhudi hizo, ugonjwa wa ukoma bado haujatokomezwa kikamilifu.