Alkhamisi, tarehe 30 Januari, 2025
Lo ni Alkhamisi tarehe 29 Rajab 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 30 Januari 2025.
Siku kama ya leo, miaka 1170 iliyopita, alifariki dunia Abdullah bin Muslim Dinawari, maarufu kwa jina la Ibn Qutaybah akiwa na umri wa miaka 63.
Ibn Qutayba alizaliwa huko Kufah, Iraq na kushika hatamu za ukadhi huko mjini Dinawari, magharibi mwa Iran. Alitabahari katika elimu ya Qur’ani, Hadithi, mashairi na fasihi.
Alimu huyo ameandiandika vitabu mbalimbali katika elimu za Kiislamu maarufu zaidi vikiwa ni “Ta’awiilu Mushkili-Qur’ani”, “Tafsiru Gharibil-Qur’an”, “Uyunul-Akhbaar”, “Maani ash-Shi’ir” na “Gharibul- Hadith.” ****
Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, kilianza kipindi cha uongozi wa Adolph Hitler, dikteta mbaguzi wa Kinazi wa Ujerumani.
Chama cha Taifa cha Kisoshalisti cha Wafanyakazi wa Ujerumani ambacho kiliasisiwa na Hitler kilishinda viti 107 vya bunge katika uchaguzi wa mwaka 1930. Adolph Hitler alijitangaza kuwa kiongozi wa Ujerumani mwaka 1934 baada ya kuwa Kansela na Rais wa nchi hiyo. Hitler aliwafanya mamilioni ya wanadamu kuwa wahanga wa malengo yake ya kibaguzi. Hatua ya Adolph Hitler ya kuivamia Poland mwezi Septemba mwaka 1939 ilichochea Vita vya Pili vya Dunia na hatimaye Ujerumani na waitifaki wake walishindwa katika vita hivyo.
Hitler alijiua mwaka 1945 baada ya Ujerumani kushindwa katika vita hivyo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 77 iliyopita kiongozi wa taifa la India na mpigania uhuru wa nchi hiyo, Mohandas Karamchand Gandhi aliuawa na kijana mmoja wa Kihindu aliyekuwa na misimamo mikali.
Gandhi alizaliwa mwaka 1869 na baada ya kukamilisha masomo alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya sheria nchini Uingereza. Mohandas Gandhi kwa muda fulani pia alikuwa kiongozi wa wanamapambano wa Kihindi huko Afrika Kusini.
Gandhi pia aliwaongoza wananchi wa India dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika kupigania ukombozi wa nchi hiyo. India ilipata uhuru mwaka 1947 chini ya uongozi wa Gandhi. ****
Katika siku kama ya leo miaka 77 iliyopita Orville Wright, mmoja wa waundaji wa ndege ya kwanza inayotumia injini duniani, alifariki dunia.
Orville alizaliwa mnamo Agosti 19, 1871 katika jimbo la Ohio huko Marekani na alikuwa mdogo kwa miaka minne kuliko kaka yake, Wilbur. Orville na Wilbur walikuwa watoto wa padri ambaye hakuweza kumudu gharama za masomo yao kutokana na umaskini. Kwa hivyo, ndugu hawa wawili, ambao walivutiwa na kazi za ufundi na utengenezaji wa injini na mashine, walianzisha warsha ya kutengeneza baiskeli.
Ndugu hawa wawili, ambao walikuwa na hamu kubwa ya kuruka angani, hatimaye walitimiza ndoto yao ya muda mrefu mnamo Desemba 17, 1903, na wakavumbua ndege ya kwanza yenye injini ulimwenguni ambayo iliruka angani kwa sekunde 59.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita gwaride la mwisho na kimaonyesho la vikosi vya majeshi ya utawala wa Shah lililokuwa na lengo la kuwatia hofu na woga wananchi Waislamu wa Iran, lilifanyika katika mitaa mbalimbali ya Tehran.
Katika gwaride hilo, wanajeshi wengi walionesha mshikamano wao na kuungana na wananchi Waislamu wa Iran na kuamua kuanza mapambano dhidi ya utawala wa kibeberu wa Shah.
