Jumatatu, tarehe tatu Februari, 2025
Leo ni Jumatatu tarehe 4 Shaabani 1446 Hijria, sawa na tarehe tatu Februari 2025.
Siku kama ya leo miaka 1420 iliyopita, yaani tarehe 4 Sha'ban mwaka 26 Hijria, alizaliwa Hadhrat Abbas Bin Ali Bin Abi Talib, mashuhuri kwa lakabu ya Abul Fadhl.
Mama yake ni Ummul-Banin, ambaye aliolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as). Abul Fadh al-Abbas alikulia katika familia ya watu adhimu kama vile baba yake Imam Ali (as), kaka zake Imam Hassan na Hussein na dada yake mtukufu Zaynab (as). Alimpenda sana kaka yake Hussein Bwana wa Mashahidi, kiasi kwamba alisabilia maisha yake katika ardhi ya Karbala kwa lengo la kumtetea yeye na risala yake kwa nguvu zake zote.
Abbas alifahamika mno kutokana na elimu, ukweli na uchaji Mungu wake. Kutabahari kwake katika elimu kuliwafanya watu wengi warejee kwake kwa ajili ya kutatuliwa masuala mbalimbali ya kielimu.
Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Abul Fadhl Abbas inajulikana hapa nchini Iran kama Siku ya Vilema wa Vita. Aidha katika siku ya kuzaliwa mtukufu huyo, watu wa Iran huwa wanawakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliosimama imara katika vita vya kulazimishwa vya utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran.

Siku kama ya leo miaka 1006 iliyopita, sawa na tarehe 4 Shaban 440 Hijiria, alifariki dunia Abu Said Abul-Khayr, mtaalamu wa elimu ya Kumjua Mwenyezi Mungu (irfan) na malenga wa Iran akiwa na umri wa miaka 83.
Abu Said alizaliwa mwaka 357 Hijiria na kujifunza elimu ya hisabati na historia ya wafalme. Aidha alitabahari katika elimu za tafsiri ya Qur’ani, Hadithi na fiqhi (sheria za Kiislamu), huku akipata elimu ya irfani kutoka kwa wanazuoni mashuhuri wa elimu hiyo wa karne ya nne na ya tano Hijiria.
Kitabu cha ‘Asraarut-Tawhid’ ni moja ya turathi za Abu Said Abul-Khayr. Aidha alipendelea sana kusoma mashairi.

Katika siku kama ya leo miaka 557 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa mashine ya uchapishaji, Johannes Gutenberg.
Mvumbuzi huyo alizaliwa nchini Ujerumani lakini alihamia Strasbourg, Ufaransa na akaanza kujishughulisha na kazi za kiufundi.
Mwaka 1443 au 1444 Gutenberg alifanikiwa kutengeneza mashine ya uchapishaji na kupiga hatua muhimu katika uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.'

Miaka 195 iliyopita katika siku kama ya leo, Ugiriki ilipata uhuru wake kutoka kwa utawala wa Othmania.
Ugiriki ambayo kijiografia ipo kusini mashariki mwa Ulaya ni moja kati ya nchi zenye tamaduni kongwe duniani. Mwaka 338 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (a.s), mfalme wa Macedonia aliivamia Ugiriki na karne moja baadaye nchi hiyo ikawa chini ya mamlaka ya utawala wa Roma na baadaye Roma ya Mashariki.
Katika kipicdi chote cha karne ya 19, Ugiriki ilishuhudia mapigano vita na vurugu za ndani na nje. Hatimaye katika siku kama ya leo nchi hiyo ikajipatia uhuru.

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, mfereji wa Suez uliokuwa ukidhibitiwa na Uingereza, ulishambuliwa na vikosi vya majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othmaniya katika Vita vya Kwanza vya Dunia.
Udhibiti wa mfereji huo wa Suez ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa pande mbili zilizokuwa zikipigana katika Vita vya Kwanza vya Dunia kutokana na ukweli kwamba, mfereji huo ndio unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu.
Uingereza ambayo haikuwa tayari kupoteza makoloni yake ya Asia, ilipigana vikali na majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othmaniya na kupata ushindi.
Mfereji wa Suez uliendelea kudhibitiwa na Uingereza hadi ulipotaifishwa na kiongozi wa Misri Gamal Abdul Nasir hapo mwaka 1956 na kufanywa kuwa mali ya taifa.

Katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, Woodrow Wilson Rais wa 28 wa Marekani alifariki dunia.
Woodrow Wilson alizaliwa 1913 na akiwa na umri wa miaka 57 alichukua hatamu za uongozi wa Rais wa Marekani. Kama walivyokuwa Marais waliomtangulia wa Marekani, na yeye alikita zaidi katika kuingilia masuala ya ndani ya Amerika ya Kati.
Kipindi cha urais wa Woodrow Wilson kilitawaliwa na uingiliaji na uvamizi wa kijeshi dhidi ya maeneo mbalimbali duniani. Nusu ya kipindi cha utawala wa Woodrow Wilson, kilishuhudia Marekani ikishughulishwa na vita. Nchi zilizoshambuliwa kijeshi na Marekani katika uongozi wa Rais Woodrow Wilson ni Haiti, Guatemala, Dominican na Cuba.

Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita wakati mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah yalipokuwa yamefika kileleni, Waziri Mkuu wa utawala wa kifalme hapa nchini Shapour Bakhtiar alifanya jitihada za kuzima vuguvugu la wananchi bila ya mafanikio yoyote.
Bakhtiar alisema katika mahojiano na vyombo vya habari kwamba, hatamruhusu Imam Khomeini kuunda serikali ya mpito.
Wakati huo uasi wa kiraia, kukimbia wanajeshi na kujiunga na safu za wananchi katika miji mbalimbali ya Iran ikiwa ni pamoja na kujiuzulu wabunge, viongozi wa ngazi za juu serikali na kadhalika viliifanya serikali ipoteze udhibiti wa mambo ndani ya nchi.
