Feb 04, 2025 02:22 UTC
  • Jumanne, 04 Februari, 2025

Leo ni Jumanne tarehe 05 Shaaban 1446 Hijria sawa na 04 Februari 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1408 iliyopita alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina.

Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku.

Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik.

Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya. 


Kaburi la Imam Sajjad, Baqii, Madina

Miaka 1133 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia tabibu na mwanakemia mtajika wa ulimwengu wa Kiislamu na mvumbuzi wa alkoholi kwa jina la Muhammad bin Zakaria Razi.

Tabibu Razi alizaliwa mwaka 251 Hijria katika mji wa Rei kusini mwa Tehran ya leo. Mwanakemia huyo mkubwa alianza kujishughulisha na kazi ya usonara na baadaye kemia. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadae Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya Sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia.

Mwanasayansi huyu Muislamu wa Iran alikuwa mtu wa kwanza kugundua alkoholi. *

Siku kama hii ya leo miaka 337 iliyopita Pierre Marivaux mwandishi wa riwaya na michezo ya kuigiza wa Kifaransa alizaliwa huko Paris nchini Ufaransa.

Pierre alianza kujishughulisha na kazi ya sanaa tangu akiwa kijana na kwa muda fulani alishiriki pia katika michezo ya kuigiza hadi pale alipoanza kuandika michezo hiyo.

Marivaux alipata umashuhuri mkubwa kutokana na ukosoaji wake katika uandishi wa riwaya. Marivaux ameacha athari nyingi za kimaandishi zikiwemo riwaya na michezo ya kuigiza ambapo miongoni mwake tunaweza kuashiria zile alizozipa majina kama ya The Prudent na Equitable Father, The Triumph of Love na The Life of Marianne.

Pierre Marivaux

Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita kulifanyika mkutano uliojulikana kwa jina la Yalta katika peninsula ya Crimea huko kusini mwa Urusi ya zamani.

Mkutano huo uliwakutanisha pamoja  viongozi wa nchi za Uingereza, Marekani na Shirikisho la Urusi ya zamani (Churchill, Roosevelt na Stalin). Mkutano huo ulifanyika baada ya kudhihiri dalili za kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia.

Lengo hasa la mkutano wa Yalta lilikuwa kujadili hali ya kisiasa na kijeshi ya nchi zilizokuwa zikipigana vita hivyo, ikiwa ni pamoja na kuainisha hatima ya ardhi zilizokuwa chini ya madola waitifaki.

Mkutano wa Yalta

Miaka 77 iliyopita katika siku kama ya leo nchi ya Sri Lanka ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza.

Nchi hiyo iliyoko kusini mashariki mwa India ilivamiwa na wakoloni wa Kireno katikati mwa karne ya 16 na baadaye wakoloni wa Kiholanzi na tangu mwaka 1798 iliunganishwa rasmi na makoloni ya Uingereza. Mapambano ya kupigania uhuru wa Sri Lanka yalianza mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Mwaka 1931 Uingereza ililazimika kutoa haki ya kutoa maoni kwa wananchi wa Sri Lanka na kuasisi baraza la kutunga sheria na baraza la utekelezaji. Hata hivyo nchi hiyo ilikuwa bado haijapata uhuru kamili katika masuala ya kigeni. Kwa msingi huo mapambano ya wananchi yaliendelezwa hadi kisiwa hicho kilipopata uhuru kamili mwaka 1948.

Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilikiri kushindwa kutabiri masuala ya Mapinduzi ya Kiislamu. Maafisa wa CIA walikiri kuwa shirika hhilo limeshindwa kutabiri matukio ya Iran. Walisema, kitu ambacho hatukukitabiri kabisa ni mtu mmoja mzee wa miaka 78 ambaye alibaidishwa nje ya nchi kwa muda wa miaka 14, kuweza kuwaunganisha kiasi chote hiki wananchi wa Iran.   

Na siku kama ya leo miaka 9 iliyopita aliaga dunia Raghib Mustafa Ghalwash qarii na msomaji Qur'ani mahiri wa Kimisri.

Ghalwash alizaliwa Julai 5 mwaka 1938 nchini Misri na kukulia katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na Qur'ani. Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa tayari amehifadhi Qur'ani nzima katika rika la ubarobaro na kuanza kusoma kitabu hicho katika hafali na majlisi mbalimbali akiwa na umri wa miaka 16.

Sheikh Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa miongoni mwa wasomaji wa Qur'ani waliofanya safari nchini Iran baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa vilivyoanzisha na Iraq dhidi ya Iran.

Qiraa na kisomo cha gwiji huyo wa Misri kilipendwa sana nchini Iran. Hatimaye Qarii huyo mashuhuri aliaga dunia alfajiri ya Alkhamisi tarehe 4 Februari mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 77 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Raghib Mustafa Ghalwash