Ijumaa, tarehe 7 Februari, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 08 Shaabani 1446 Hijria sawa na tarehe 7 Februari 2025.
Siku kama ya leo miaka 546 iliyopita, alizaliwa Thomas More, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchini Uingereza.
Mwanzoni More alisomea elimu ya sheria na baada ya kujiunga bungeni akapewa mazingatio na malkia wa wakati huo na kutunukiwa hadhi ya Ulodi. Hata hivyo Thomas More alitofautiana kinadharia na mfalme wa wakati huo wa Uingereza na hivyo akatiwa jela na kuhukumiwa kifo.
Hatimaye More akanyongwa mnamo tarehe sita Julai mwaka 1535 Miladia akiwa na umri wa miaka 57.
Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita, alizaliwa mjini Newcastle Edward Granville Browne, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, mtafiti na fasihi wa nchini Uingereza.
Awali Browne alisomea fani ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Cambridge na kuhitimu masomo yake chuoni hapo. Hata hivyo kutokana na kupendelea kwake kusoma tamaduni za Mashariki mwa dunia alifanya safiri nchini Iran akiwa na umri wa miaka 25. Aidha mtafiti huyo aliitaja lugha ya Kifarsi kuwa njia bora ya kunakili fikra na tamaduni za Wairani kuelekea maeneo mengine ya dunia.
Ni kwa msingi huo ndio maana akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na historia na utamaduni wa Wairani. Mwishoni Edward Granville Browne alijikita katika kufundisha lugha ya Kifarsi na Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Cambridge, na kufariki dunia mwaka 1926 akiwa na umri wa miaka 54. ***
Miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi dogo ya Grenada iliyoko katika Amerika ya Kaskazini ilijipatia uhuru.
Kisiwa hicho kiligunduliwa mwaka 1498 na Christopher Columbus mvumbuzi wa Kihispania na ikaunganishwa na nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1674 Ufaransa ikaidhibiti Grenada.
Baada ya takribani karne moja yaani mwaka 1783, Waingereza waliifanya Grenada kuwa koloni lao na hali hiyo ikadumu kwa takribani karne mbili. Hatimaye mwaka 1974 na katika siku kama ya leo, Grenada ikajikomboa na kujipatia uhuru. ****

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita wananchi wa Iran walifanya maandamano makubwa katika miji mbalimbali ya Iran na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano hadi kuuangusha utawala wa Shah.
Mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran waliandamana katika siku kama hii wakijibu wito wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu aliyewataka waiunge mkono serikali ya muda ya Mapinduzi.
Katika upande mwingine maafisa na vikosi vya Jeshi la Anga la Iran waliokuwa katika sare zao za kijeshi, walielekea kwa Imam na kutangaza mshikamano wao na Mapinduzi ya Kiislamu na uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini. Katika mazungumzo hayo, Imam Ruhullah Khomeini aliwaambia wanajeshi hao kwamba walikuwa watumishi wa utawala wa kitaghuti na sasa wamejiunga na Qur'ani.
Hatua ya vikosi vya Jeshi la Anga la Iran ya kutangaza utiifu wao kwa Imam Khomeini iliukasirisha sana utawala wa Shah.