Feb 20, 2025 02:32 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 20 Februari, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Sha'ban 1446 Hijria sawa na Februari 20 mwaka 2025.

Katika siku kama ya leo miaka 940 iliyopita alizaliwa Abdulkarim bin Muhammad Sam'ani maarufu kwa lakabu ya Tajul Islam, faqih, mpokezi wa Hadithi na mwanahistoria mtajika wa karne ya sita Hijria huko katika mji wa Marw kusini mashariki mwa Tukimanistan ya sasa na Khurasan kubwa ya zamani.

Sam'ani alipitisha miaka mingi ya umri wake kwa kufanya safari katika nchi mbalimbali kama vile Iran, Sham, Hijaz na nyinginezo na kunufaika na bahari kubwa ya wasomi wa kila sehemu aliyokwenda.

Kitabu maarufu cha msomi Sam'ani ni kile alichokita kwa jina la " al Ansaab."

Katika siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, vita kati ya Ufaransa na wapigania uhuru wa Mexico vilimalizika kwa ushindi wa Ufaransa na kushika hatamu za uongozi mwanamfalme wa Austria, Maximilian.

Katika vita hivyo vilivyoendelea kwa kipindi cha miaka 5, awali Ufaransa iliungana na Uhispania na Uingereza na baada ya muda mfupi nchi hizo mbili zilijitenga na Ufaransa ambayo iliendeleza vita dhidi ya wapigania uhuru wa Kimexico waliokuwa wakiongozwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Benito Juárez.

Benito Juárez aliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni wa Kifaransa hata baada ya kurudi nyuma na kukimbilia katika maeneo ya milimani ya Mexico. Kiongozi huyo hatimaye alifanikiwa kuangusha utawala wa Maximilian akisaidiwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo.   

Benito Juárez

Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Februari 1947, Uingereza hatimaye ilikubali kuipatia India uhuru wake baada ya kuikoloni nchi hiyo kwa zaidi ya karne mbili.

Uhuru wa India ulipatikana kutokana na mapambano ya muda mrefu yaliyoongozwa na Mahatma Gandhi. Katika kipindi chote cha utawala wake wa kikoloni huko India, Uingereza ilipora utajiri na maliasili za nchi hiyo na kuwasababishia hasara kubwa raia wa India.

Mwezi Agosti mwaka huohuo India ikajipatia rasmi uhuru wake na ikagawanyika katika nchi mbili za India na Pakistan.   

Na tarehe 20 Februari miaka 9 iliyopita aliaga dunia Sheikh Ahmad A'mir, qari na msomaji maarufu wa Qur'ani tukufu wa Misri. Alizaliwa mwaka 1927 katika eneo la Salihiyah huko mashariki wa Misri na kuhifadhi Qur'ani yote akiwa bado mdogo. Baadaye alijiunga na jeshi na mwaka 1963 alifanya kazi kwenye radio ya nchi hiyo.

Qari huyo mashuhuri wa Misri alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kusoma Qur'ani na alifika nchini Iran mara kadhaa katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu kama jaji wa mashindano hayo. Mara ya mwisho msomaji huyo mkubwa wa Qur'ani alitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka 2013 na kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu.

Baada ya mashindano hayo, Sheikh Ahmada A'mir alisoma Qur'ani katika majlisi iliyohudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei wakati huo akiwa na umri wa miaka 86. Qiraa ya Sheikh Ahmad A'mir katika majlisi hiyo iliwagusa sana hadhirina na kuwafanya wengi wabubujikwe na machozi.

Sheikh Ahmad A'mir