Feb 24, 2025 03:12 UTC
  • Jumapili, 23 Februari, 2025

Leo ni Jumapili 24 Shaaban 1446 Hijria mwafaka na 23 Februari 2025

Leo tarehe 5 mwezi wa Esfand kwa kalenda ya Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi na kumkumbuka mwanafikra mkubwa wa Kiislamu na Kiirani, Khajah Nasiruddin Tusi.  Sikuu hii inajulikana pia katika kalenda ya Iran kwa jina la Siku ya Uhandisi. Abu Jaafar Muhammad bin Muhammad maarufu kwa jila na Khajah Nasiruddin Tusi aliyepewa laqabu ya "mwalimu wa wanadamu" na Muhaqqiq Tusi alizaliwa mwaka 597 Hijria katika eneo la Tusi kaskazini mashariki mwa Iran. Katika kipindi cha maisha yake, mwanafalsafa, mwanahisabati, mnajimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiirani aliasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kufuatilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe huko kaskazini magharibi mwa Iran. Aalimu huyo aligundua namna mpya za kutumia saa ya jua kwa ajili ya kituo hicho. Kituo hicho kilikuwa na suhula muhimu zaidi ambazo hazikushuhudiwa katika nchi za Magharibi kwa kipindi cha miaka 300 baada yake. Vilevile alikusanya vitabu vya elimu na taaluma mbalimbali kutoka Iraq, Sham, kaskazini mwa Afrika na maeneo ya kandokando mwa Iran na kuasisi maktaba kubwa iliyokuwa na zaidi ya vitabu laki nne. Khajah Nasiruddin Tusi alifariki dunia mwaka 672 Hijria akiwa na umri wa miaka 75 na kuzikwa katika mji wa Kadhimain nchini Iraq. ***

 

Siku kama ya leo miaka 226 iliyopita, baada ya Napoleon Bonaparte, kamanda wa jeshi la Ufaransa kuidhibiti Misri, alianza kufanya mashambulio dhidi ya Sham, ambayo wakati huo ilikuwa ikundwa na nchi za Syria, Jordan, Lebanon na Palestina. Mashambulio ya Bonaparte dhidi ya Misri ilifanyika kwa lengo la kutoa pigo kwa Uingereza iliyokuwa mkoloni wa Misri. Lakini sababu ya mashambulio ya Napoleon Bonaparte dhidi ya Sham iliyokuwa sehemu ya ardhi ya utawala wa Othmania, ni hatua ya mfalme wa utawala wa Othmania ya kutangaza vita dhidi ya Ufaransa. Katika mashambulio hayo, licha ya kuwa awali Bonaparte alipata ushindi, lakini baadaye alilazimika kuacha vita na kurejea kwao kutokana na uungaji mkono wa Uingereza na Urusi kwa utawala wa Othmania bila kusahau kuharibika hali ya mambo ndani ya Ufaransa. 

 

Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita, alifariki dunia Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mar'ja' mashuhuri wa Kiislamu.  Alizaliwa mwaka 1230 katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini na kupata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama Sheikh Murtadha Ansari. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa ikihodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni. 

 

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, Aliaga dunia Paul Claudel mwandishi, mshairi na mwanasiasa wa Kifaransa. Claudel alizaliwa 1868 na akiwa katika rika la ujana alijiunga na shule ya elimu ya siasa.  Mpaka mwaka 1935 Claudel alikuwa mfanyakazi katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ufaransa na alisafiri katika mataifa mbalimbali kutekeleza majukumu yake ya kikazi. Hata hivyo kuanzia mwaka huo alichukua muelekeo wa fasihi. Msomi huyyo alikuwa na harakati katika taaluma mbalimbali za fasihi kama mashairi, visa na uandishi na maigizo.

 

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, yaani sawa na tarehe 23 Februari 1970 Miladia, mfumo wa utawala nchini Guyana ulibadilishwana kuwa wa jamhuri na siku hii inajulikana nchini humo kuwa Siku ya Jamhuri. Pwani ya Guyana ilivumbuliwa na wavumbuzi wa Kihispania. Mwanzoni mwa karne ya 17 Miladia, Uingereza iliikoloni nchi hiyo hadi mwaka 1966 ilipojipatia uhuru wake.