Ijumaa, tarehe 7 Machi, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 6 Ramadhani mwaka 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Machi mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 983 iliyopita, yaani tarehe 6 Ramadhani mwaka 463 Hijria Qamaria, alifariki dunia Hamza Bin Abdul Aziz Daylami, ambaye pia alifahamika kwa jina la Sallar, mwanachuoni mkubwa wa karne ya 5 Hijria Qamaria katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran.
Alifahamika kwa lakabu ya Abu Ali. Miongoni mwa kazi muhimu za msomi huyo wa Kiirani ni vitabu vilivyokuwa na anwani za "Al-Marasimul Alawiyya wal Ahkaamu Nabawiyyah" na mkusanyiko wa vitabu kumi alioupa jina la "Jawamiul Fiqhi".
Vitabu vingine vilivyochapishwa vya mwanachuoni huyo ni pamoja na "Al-Abwaabu wal Fusul", na "Taqrib" vilivyojadili masuala ya fiqhi.

Katika siku kama ya leo miaka 751 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa wa Kitaliano Thomas Aquinas.
Alizaliwa mwaka 1225 katika mji wa Napoli na kupata elimu ya dini katika mji huo hadi chuo kikuu. Mwanafikra huyo alibuni falsafa makhususi na kutambua kwamba saada na ufanisi mkubwa zaidi wa mwanadamu ni kupiga hatua za kuelekea kwenye ukamilifu wa kiroho na kwa Mwenyezi Mungu.
Aquinas kama alivyokuwa Aristotle, aliamini kuwa ndani ya nafsi ya kila mwanadamu kuna nguvu inayoweza kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiroho. Vilevile aliamini kwamba teolojia haipingani na sayansi kwani kila moja kati ya viwili hivyo inataka kujua hakika na kweli.
Itikadi za Aquinas na misimamo yake ya kutumia akili na mantiki ambayo ilikuwa ikipingwa vikali na kanisa katika karne za kati, ilisaidia sana kueneza elimu.

Tarehe 7 Machi miaka 260 iliyopita alizaliwa Nicephore Niepce mwanakemia wa Kifaransa na mmoja wa waasisi wa sanaa ya upigaji picha.
Niepce alikuwa mtu wa kwanza aliyefanikiwa kupiga picha ya kwanza duniani. Baada ya hapo, Nicephore alitengeneza kamera ya kupiga picha kwa kushirikiana na marafiki zake. Mwanakemia huyo wa Ufaransa aliaga dunia mwaka 1833.

Siku kama hii ya leo miaka 89 iliyopita vikosi vya jeshi la Ujerumani ya Kinazi vilifanya mashamulizi ya kwanza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia.
Wanajeshi wa Ujerumani walipuuza makubaliano ya Warsaw na Locarno kwa amri ya Adolph Hitler na hivyo kuingia eneo la Ranani.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Locarno na Warsaw, eneo la Ranani lililokuwa likigombaniwa kati ya Ufaransa na Ujerumani lilitangazwa kuwa eneo lisiloegamea upande wowote. Hata hivyo jeshi la Ujerumani liliamua kuliteka na kulikalia kwa mabavu eneo hilo katika siku kama hii ya leo.
