Jumamosi, Machi 29, 2025
Leo ni Jumamosi tarehe 28 Ramadhani 1446 Hijria sawa na tarehe 29 Machi mwaka 2025 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1174 iliyopita aliaga dunia Abu Ma'ashar Balkhi mmoja wa wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya hadithi wa Kiirani.
Alielekea Baghdad mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Katika zama zake, Abu Ma'ashar Balkhi alikuwa mnajimu mashuhuri wa Kiislamu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Mad'khal al-Kabir na al-Mawalid as-Saghirah.

Siku kama ya leo miaka 452 iliyopita, yaani tarehe 29 Machi 1573 Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa alitoa amri ya kihistoria iliyojulikana kama amri ya uhuru, ambayo ilikuwa kwa maslahi ya Wakristo wa madhehebu ya Protestanti.
Kwa mujibu wa amri hiyo, Waprotestanti wa Ufaransa ambao walijipatia ushindi kwenye vita vya nne dhidi ya Wakatoliki wa nchi hiyo, walikuwa huru kufanya sherehe, ibada na misa zao nchini humo.
Vita vya nne vya kidini kati ya Wakatoliki na Waprotestanti vilianza tarehe 16 Julai mwaka 1572 na vilikuwa maarufu kwa jina la Vita vya La Rochelle.

Miaka 348 iliyopita katika siku kama ya leo vita baina Poland na Ufalme wa Othmania vilifikia tamati kwa ushindi wa Ufalme huo na kutekwa sehemu ya ardhi ya Ukraine iliyokuwa chini ya utawala wa Poland.

Siku kama ya leo miaka 253 iliyopita, alifariki dunia Emmanuel Swedenborg, aliyekuwa mwanafikra mkubwa na msomi wa Sweden.
Swedenborg alizaliwa mwaka 1688 na baada ya kubobea kwenye taaluma ya hesabati, aliweza kuwa mhandisi mahiri nchini humo. Swedenborg hakutosheka na elimu hiyo na badala yake akaongeza juhudi kubwa na kutokea kuwa mtaalamu pia kwenye elimu ya falsafa na irfani. Msingi wa falsafa ya msomi huyo ulikuwa kujitenga na dunia ya kimaada na kuingia zaidi katika ulimwengu wa kimaanawi.
Kwa msingi huo Swedenborg aliamini kuwa kadiri mwanadamu anavyosafisha roho yake ndivyo anavyomuelewa na kumjua zaidi Mwenyezi Mungu. Mtaalamu huyo aliandika vitabu zaidi ya 50 kwa ajili ya kuweka wazi falsafa yake.

Katika siku kama hii ya leo miaka 123 iliyopita sawa na tarehe 29 Machi mwaka 1902 alizaliwa mwandishi wa Kifaransa, Marcel Ayme.
Awali Ayme alisomea uhandisi, hata hivyo aliachana na taaluma hiyo kutokana na kupatwa na maradhi. Baadaye alijishughulisha na uandishi wa magazeti na taratibu akaanza kujihusisha na uandishi wa riwaya ambapo alitokea kuwa mashuhuri katika uwanja huo.
Marcel Ayme ameandika vitabu kadhaa kama "Beautiful Image", na "The Green Mare".
