Jumanne, tarehe 8 Aprili, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 9 Shawwal 1446 Hijria sawa na Aprili 8 mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 1336 iliyopita katika siku kama ya leo, Ibn Sirin mpokezi wa hadithi na faqihi mashuhuri wa karne ya pili Hijria aliaga dunia. Ibn Sirin alizaliwa Basra kusini mwa Iraq.
Msomi huyo wa Kiislamu alitoa umuhimu mkubwa kwa hadithi za Mtume Muhammad SAW na alikuwa mahiri katika kuhifadhi na kunukuu hadithi. Alikutana na masahaba 30 wa Mtume Muhammad (saw).
Ibn Sirin ameacha vitabu na makala nyingi zilizoandikwa kwa lugha mbalimbali. Kutokana na hali hiyo wataalamu wengi wa hadithi wanatilia maanani sana hadithi zilizopokelewa na Ibn Sirin.
Hii leo vitabu mbalimbali na kwa lugha tofauti vimeandikwa kutoka kwa msomi huyo. Ibn Sirin anafahamika pia kwa uhodari wake wa kufasiri ndoto.

Katika siku kama ya leo miaka 166 iliyopita inayosadifiana na tarehe 8 Aprili mwaka 1859, alizaliwa Edmund Husserl, msomi wa hisabati na falsafa wa nchini Austria.
Husserl alielekea Ujerumani kwa ajili ya kujiendeleza kielimu ambapo akiwa huko alifanikiwa kufikia daraja ya Uprofesa. Kadhalika Edmund Husserl alifanya utafiti mwingi kuhusiana na elimu ya falsafa. Husserl alitambuliwa pia kuwa mwasisi wa kanuni ya Phenomenology katika falsafa, ambayo ilikuwa na taathira kubwa kwa wanafalsafa wa Kimagharibi. Aidha aliamini kwamba, lazima falsafa iambatane na hisabati, kama ambavyo aliamini kuwa dunia lazima iwe nzuri na ya kuvutia.
Ameacha athari mbalimbali ikiwemo 'Falsafa ya Hisabati' 'Uchunguzi wa Kimantiki' na vitabu vingine.

Miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo, ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel ziliishambulia shule ya msingi ya Bahrul Baqar iliyoko umbali wa kilomita 80 Kaskazini mwa mji wa Cairo.
Katika mashambulizi hayo ya kutisha watoto 46 waliokuwa wakisoma shuleni hapo waliuawa. Mashambulizi hayo ya kikatili yaliibua hasira ya watu katika nchi mbalimbali duniani. Inasemekana kuwa, kwa muda wa miezi mitatu ya awali ya mwaka 1970 ndege za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia maeneo ya kiraia huko Kaskazini Mashariki mwa Misri.
Tarehe 12 mwezi Februari mwaka huohuo Wazayuni pia walikishambulia kiwanda kimoja katika eneo hilo na kuua pamoja na kuwajeruhi wafanyakazi 168. Kadhalika Wazayuni waliwaua watu 12 katika mashambulizi dhidi ya mji wa al-Mansura ulio Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo tarehe 31 mwezi Machi mwaka huohuo wa 1970.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita sawa na tarehe 8 Aprili 1980, utawala wa Baathi nchini Iraq uliwaua Shahidi Sayyid Muhammad Baqir-Sadr na dada yake, Bintul Huda.
Sayyid Sadr alijifunza Qur'ani Tukufu na elimu nyingine za kidini akiwa mdogo na kupata daraja ya ijtihadi akiwa kijana. Alikuwa mmoja wa walimu wakubwa wa chuo cha kidini mjini Najaf, Iraq kiasi kwamba nadharia zake katika elimu ya usulu fiqhi zilipewa umuhimu mkubwa na wasomi wengine wa Kiislamu.
Msomi huyu aliyekuwa na uelewa na uwezo wa hali ya juu wa kielimu, aliuarifisha Uislamu kwa njia sahihi. Kwa kipindi kifupi Ayatullah Sadr aligeuka na kuwa kiongozi wa kifikra na kisiasa wa wananchi wa Iraq na kuyapa mwelekeo mpya mapambano ya wananchi wa nchi hiyo. Baada ya muda fulani utawala wa nchi hiyo ambao ulihisi hatari kutokana na harakati za Ayatullahi Sadr hivyo ulimtia mbaroni na kisha kumuua shahidi mwanazuoni huyo mashuhuri pamoja na dada yake, licha ya malalamiko makubwa ya maulama na wananchi Waislamu wa Iraq.
Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kitabu cha "Uchumi Wetu", "Hamasa ya Nuru", "Falsafa Yetu", "Mwanadamu wa Leo na Matatizo ya Kijamii", na "Ukhalifa wa Mwanadamu na Ushuhuda wa Mitume".

Miaka 12 iliyopita katika siku kama ya leo Margaret Hilda Thatcher, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza alifariki dunia.
Margaret Thatcher alikuwa mwanachama wa Chama cha Wahafidhina nchini Uingereza ambapo mwaka 1975 alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama hicho. Mwaka 1990 alikuwa kiongozi wa Chama cha Wahafidhina nchini Uingereza na Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Thatcher ndiye mwanamke wa kwanza wa Uingereza kushikilia uongozi wa chama na Uwaziri Mkuu kwa pamoja.
