Jumapili, 11 Mei, 2025
Leo ni Jumapili 13 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1446 Hijria mwafaka na 11 Mei 2025 Miladia.
Miaka 680 iliyopita katika siku kama ya leo, Qutb al-Din Muhammad bin Muhammad al-Razi alifariki dunia. Alizaliwa Varamin, eneo la Ray, na kwa kuwa alikulia huko, alijulikana kama Razi. Qutb al-Din alikuwa mmoja wa wanafunzi wakubwa wa Allamah al-Hilli. Qutb Razi alimtumikia Sultan Abu Said na waziri wake, Khwaja Ghiyath al-Din Muhammad, kwa muda, na aliandika vitabu viwili, "Sharh Shamsiyah" na "Sharh Mutala'a kwa jina la waziri huyo. Baada ya kifo cha Sultan Abu Said, alikwenda Shamu na akafa huko Damascus.

Katika siku kama ya leo miaka 329 iliyopita, alifariki dunia mwandishi na mwanafikra wa Kifaransa, Jean de La Bruyère. De la Bruyère alizaliwa mwaka 1645 Miladia, na kuwa wakili baada ya kutabahari katika elimu ya sheria. Hata hivyo baadaye aliachana na kazi ya uwakili na akaanza kufanya kazi serikalini, huku akijifunza masuala ya maadili na tafakuri ya mwanadamu katika zama zake. Mwandishi huyo wa Kifaransa ameandika vitabu vingi vinavyohusu utamaduni, mila na mienendo ya mwanadamu. Kadhalika ametoa mchango mkubwa katika uga wa fasihi ya Kifaransa.

Tarehe kama ya leo miaka 161 iliyopita alizaliwa Ethel Lilian Voynich mwandishi wa Ki-Ireland. Akiwa na umri wa miaka 21 Bi Lilian alielekea Russia na kusoma fasihi ya lugha ya Kirusi. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanza taratibu kuwa na shauku na fani ya uandishi na fasihi ya lugha. Bi Ethel Lilian aliaga dunia mwaka 1960.

Siku kama ya leo, miaka 158 iliyopita, sawa na tarehe 11 mwezi Mei mwaka 1867, iliundwa nchi ya Magharibi mwa bara Ulaya ya Luxembourg. Awali Luxembourg ilifahamika kama Lutxenbourg katika karne ya 10 hadi 15, ikiwa sehemu ya Utawala wa Roma. Hadi katikati ya karne ya 19, nchi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na serikali na watawala wa madola yaliyokuwa na nguvu na ushawishi wakati huo Ulaya. Luxembourg ambayo imezungukwa na Ubelgiji, Ufaransa na Ujerumani, ilitangazwa kuwa nchi huru katika Kongamano la London lililofanyika Mei 11 mwaka 1867 katika mji huo mkuu wa Uingereza na kuanza kutambulika kimataifa.

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, Salvador Felipe Dali, mchoraji na mchongaji wa sanamu za mawe na mtaalamu wa sanaa ya maandishi au Graphic Arts wa Kihispania alizaliwa. Alianza kuonyesha kipaji chake katika sanaa ya uchoraji akiwa kijana mdogo na kwa muda mfupi tu akawa mashuhuri kimataifa. Salvador Felipe Dali alikuwa na kipaji cha aina yake na ubunifu katika taaluma hizo na ndiye anayehesabiwa nchini Uhispania kuwa mwasisi wa uchoraji wa kisasa. Mwanasanaa huyo stadi aliaga dunia mwaka 1989.

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita kituo cha kwanza cha kurushia matangazo ya televisheni kwa jina la Nipkow kilianza kazi rasmi katika mji wa Berlin huko Ujerumani, hatua ambayo iliwawezesha watu kuanza kutumia runinga au televisheni. Kituo hicho cha kwanza cha matangazo ya televisheni kilipewa jina la Nipkow kwa shabaha ya kumuenzi Paul Gottlieb Nipkow ambaye alikuwa miongoni mwa wavumbuzi asili wa televisheni. Nipkow alivumbua njia ya kubadili picha na kuwa mawimbi na kisha kuyarejesha mawimbi hayo katika sura ya picha.

Miaka 85 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya pamoja ya Ufaransa na Uingereza yaliwasili nchini Ubelgiji kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo iliyokuwa ikikabiliwa na uvamizi wa vikosi vya Ujerumani ya Kinazi. Hatua hiyo ya Ufaransa na Uingereza ya kuiunga mkono Ubelgiji ilikuwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwako baina ya nchi hizo. Licha ya kuweko muungano huo wa kijeshi, vikosi vya Ujerumani ya Kinazi mbali na kuyashinda majeshi ya Ubelgiji vilivishinda pia vikosi vya pamoja vya Uingereza na Ufaransa na kuikalia kwa mabavu ardhi yote ya nchi hiyo.
