Jumamosi, 14 Juni 2025
Leo ni Jumamosi 18 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1446 Hijria sawa na 14 Juni 2025 Miladia.
Siku kama hii ya leo miaka 1436 iliyopita Mtume Muhammad (SAW) akiwa katika safari yake ya mwisho ya Hija, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilifanyika katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir Khum katika makutano ya njia ya Makka na Madina. Siku hiyo Mtume SAW alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Twalib na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui." Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika Hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama.

Siku kama ya leo miaka 774 iliyopita, alifariki dunia Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mtaalamu wa hesabati na nujumu na msomi mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Nasiruddin Tusi aliishi katika kipindi cha Hulagu Khan Mongol na aliasisi kituo kikubwa na cha kwanza cha sayansi ya nujumu huko Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran. Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaq Naaswiri’, ‘Awsaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat.

Katika siku kama ya leo miaka 289 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa kwa jina la Charles Augustin de Coulomb. Msomi huyo alianza kufundisha masomo katika nyanja za umeme na sumaku baada ya kuhitimu masomo yake na kuandika vitabu vingi katika uwanja huo. Mbali na kufundisha, mwanafizikia Augustin de Coulomb aliendelea pia kufanya utafiti na hatimaye akafanikiwa kubuni kanuni katika sayansi ya fizikia iliyojulikana kwa jina lake. De Coulomb aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70. ***

Tarehe 18 Dhulhija miaka 232 iliyopita alizaliwa faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasaail na Makaasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.

Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, wanajeshi wa Misri wakiongozwa na Kamanda Muhammad Ali Pasha waliishambulia Sudan na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Wakati huo huo Waingereza pia walilishambulia eneo la kusini mwa Sudan na kulikalia kwa mabavu. Hata hivyo wananchi wa Sudan wakiongozwa na Mahdi al Sudani mwaka 1881 walianzisha harakati ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Misri na Uingereza na mwaka 1885 wakafanikiwa kutoa pigo kubwa kwa vikosi vamizi vya Misri na Uingereza na hivyo kuyakomboa maeneo hayo. ***

Miaka 195 iliyopita katika siku kama ya leo wanajeshi wa Ufaransa waliwasili katika pwani ya Algeria huko kaskazini mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa oparesheni za kijeshi za Ufaransa zilizokuwa na lengo la kuikalia kwa mabavu na kuikoloni Algeria. Hata hivyo uvamizi huo wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria ulikabiliwa na mapambano makubwa ya wananchi dhidi ya maghasibu wa Kifaransa. Mapambano hayo ya kupigania ukombozi ya wananchi wa Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa yalipamba moto baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Hatimaye mwaka 1962 Rais wa wakati huo wa Ufaransa alilazimika kuipatia Algeria uhuru kamili kufuatia mashinikizo ya mapambano ya wananchi wa Algeria na upinzani wa fikra za waliowengi ndani ya Ufaransa kwenyewe na kimataifa. ***

Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita mto mrefu na mkubwa zaidi wa Asia wa Yangtze Kiang ulivunja kingo zake na kusababisha mafuriko ya kutisha. Mvua kali za msimu zilizonyesha zilisababisha mawimbi na mafuriko makubwa yaliyovunja kingo na mabwawa yote ya kandokando ya mto huo. Maji hayo yaligubika ardhi ya majimbo 8 ya China. Inasemekana kuwa tukio hilo kubwa liliathiri karibu watu milioni 50 wakiwemo waliopoteza maisha, kupoteza makazi, uharibifu wa mashamba, wale waliofariki dunia kutokana na maradhi ya aina mbalimbali na kadhalika. ***

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo, Wajumbe 120 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliwasilisha hoja ya kuto9kuwa na ustahiki wa kuongoza Rais Bani Sadr. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya muqawama wa wananchi dhidi ya uvamizi wa Wanajeshi wa Baathi wa Iraq katika mipaka ya vita dhidi ya Iran kuanza kusambaratika kutokana na kukosa uungwaji mkono wa lazima kutoka kwa Bani Sadr kama Amiri Jeshi Mkuu, na kufikia kilele hitilafu za Rais na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Idara ya Mahakama na taasisi za kimapinduzi zilifikia kilele chake. Hata nasaha za Imamu Khomeini za kuondoa hitilafu hizo nazo hazikufua dafu. Baada ya kupasishwa hoja hiyo katika Bunge uamuzi huo uliwasilishwa kwa Imam Khomeni ambaye naye aliudhinisha na hivyo Bani Sard akaondolewa katika wadhifa wa urais. Kuondolewa Bani Sadr, kulipelekea kung'olewa moja ya mizizi mikuu ya njama na hitilafu za ndani na Bani Sadr akakimbia nchi na kuomba hifadhi nchini Ufaransa.
