Jul 05, 2025 03:15 UTC
  • Jumamosi, 5 Julai, 2025

Leo ni Jumamosi 9 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria mwafaka na 5 Julai 2025 Miladia.

Tarehe 14 Tir katika kalenda ya Iran imepewa jina la Siku ya Kalamu. Kwa hakika kalamu huhifadhi elimu, maarifa na ni mlinzi wa fikra za wanazuoni na wasomi na hivyo ni kiunganishi cha kifikra na daraja la mawasiliano baina ya watu wa zamani na wa leo. Hata mawasiliano baina ya mbingu na ardhi yamepatikana kupitia kalamu. Hivyo basi kalamu ni mtunza siri wa mwanadamu na hazina ya elimu na mkusanyaji wa tajiriba za karne nyingi. Na kama tunaona katika Qur’ani Mwenyezi Mungu ameapa kwa kalamu kwa kusema: "Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo". Hilo linatokana na umuhimu wa kalamu, kwani kiapo mara nyingi hufanywa kwa jambo au kitu ambacho kina thamani na chenye hadhi na heshima kubwa.

Siku ya Kalamu

 

Leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, ni siku ya Tasua' yaani tarehe tisa Mfunguo Nne Muharram. Katika siku kama hii mwaka 61 Hijria wakati majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo kwa Swala na kunong'ona na Mola wake. Usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ''Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.'' Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri la kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao. Usiku huo wa kuamkia Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi, lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata dakika moja. 

Siku ya Tasua

 

Siku kama ya leo miaka 214 iliyopita, nchi ya Venezuela ilijitangazia uhuru wake na kwa sababu hiyo, tarehe 5 Julai, hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Tangu mwanzoni mwa karne ya 16, na kwa kipindi cha karne tatu Venezuela ilikuwa chini ya ukoloni wa Uhispania. Katika kipindi cha ukoloni huo, raia wa nchi hiyo walipatwa na matatizo mengi, kiasi kwamba makumi ya maelfu ya Wahindi Wekundu ambao ni raia asili wa taifa hilo waliuawa na mahala pao kuchukuliwa na Wahispania. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, mapambano ya wananchi yalianza chini ya uongozi wa Francisco Miranda na kuzaa matunda katika siku kama ya leo mwaka 1811.

Bendera ya Venezuela

 

Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, alifariki dunia Joseph Nicéphore Niépce, mvumbuzi wa kamera. Niépce alifanikiwa kusajili kwa mara ya kwanza uvumbuzi huo, mnamo mwaka 1826, baada ya kufanya majaribio kadhaa ya kielimu katika uwanja huo.   

Joseph Nicéphore Niépce

 

 Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, wananchi wa Algeria walipata uhuru dhidi ya wavamizi wa Ufaransa baada ya mapambano makali na ya muda mrefu na wavamizi hao. Ufaransa iliikalia kwa mabavu Algeria kwa kutegemea jeshi lake kubwa mnamo mwaka 1830. Kwa kipindi cha miaka 130 ya kukoloniwa taifa hilo, raia wa Algeria waliasisi harakati kadhaa za kupigania uhuru zilizokuwa zikiongozwa na Amir Abdulqadir al Jazairi, ambazo hata hivyo zilikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa jeshi la Ufaransa. Hata hivyo harakati hizo zilishika kasi zaidi na kuzaa matunda baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kujipatia uhuru wake miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo. 

Bendera ya Algeria

 

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq alifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Zulfiqar Ali Bhutto nchini Pakistan. Muhammad Zia-ul-Haq alitwaa madaraka yote ya waziri mkuu na rais wa Jamhuri ya Pakistan na mbali na kuwanyonga Zulfiqar Bhutto na wapinzani wake wengine, alivunja mabunge ya nchi hiyo na kusimamisha shughuli zote za vyama vya siasa nchini Pakistan. Zia-ul-Haq aliuawa katika ajali ya ndege akiwa na maafisa kadhaa wa jeshi la Pakistan, na utawala wake ukakomea hapo.   

Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq