Jumapili, 20 Julai, 2025
Leo ni Jumapili 24 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 20 Julai 2025.
Miaka 215 iliyopita katika siku kama ya leo, uhuru wa Colombia ulitangazwa rasmi. Colombia iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 na Wahispania na kuanza kukoloniwa. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 18, harakati za kupigania uhuru za wananchi wa nchi hiyo ziliongezeka na hatimaye harakati hizo kuzaa matunda katika siku kama ya leo. Hatua ya Napoleon Bonaparte ya kuikalia kwa mabavu Uhispania, ilizipatia fursa nzuri nchi makoloni ya Uhispania ikiwemo Colombia kuzidisha mapambano ya ukombozi. ***

Katika siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, Georg Friedrich Bernhard Riemann, mwanahisabati wa Kijerumani aliaga dunia baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu. Georg Friedrich alizaliwa mwaka 1826 katika mji wa Hanover nchini Ujerumani na baada ya kumaliza masomo yake ya awali aliendelea na masomo ya hisabati. Alipofikisha umri wa miaka 28 Bernard Riemann alikuwa tayari ni mhadhiri wa Chuo Kikuu katika uwanja huo wa hisabati. ***

Miaka 88 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Guglielmo Marconi mvumbuzi wa radio wa Kiitalia akiwa na umri wa miaka 63. Guglielmo alizaliwa mwaka 1874 huku akiwa mtoto wa mfanyabiashara mmoja wa Kiitalia. Marconi alipenda sana kujifunza masuala ya ufundi na sanaa tangu akiwa kijana mdogo ambapo alianza utafiti wa mawimbi ya sauti. Marconi hatimaye alifanikiwa kuvumbua radio baada ya utafiti wake huo na baadaye akaikamilisha bila ya kutumia waya. ***

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika mwezini. Katika siku hiyo wanaanga wa Kimarekani Neil Armstrong na Edwin Aldrin walitumia chombo cha kusafiria katika anga za mbali kwa jina la Apolo- 11 na kufika mwezini na baadaye wakarejea duniani huku wakiwa na sampuli za mawe na udongo walizokuja nazo katika safari hiyo. Kwa utaratibu huo juhudi kubwa za mwanadamu zilizokuwa zikifanywa kwa muda mrefu kwa lengo la kufikia mwezini zikawa zimezaa matunda. ***

Katika siku kama ya leo miaka 51 iliyopita , wanajeshi wa Uturuki walivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Cyprus, mashariki mwa kisiwa hicho. Tangu kale Waturuki na Wagiriki wa Cyprus walikuwa wakizozana juu ya namna gani pande mbili hizo zigawane mamlaka ya nchi hiyo. ***

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, jeshi la mtawala wa wakati huo wa Iraq, dikteta Saddam Hussein lilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya maeneo ya kusini ya Iran. Mashambulio hayo yalianza siku nne tu baada ya Iran kulikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lililokuwa limepasishwa takribani mwaka mmoja kabla, lilisisitiza juu ya usitishaji vita, liliuarifisha utawala vamizi, likataka kulipwa fidia waathiriwa wa hujuma hiyo, kubadilishana mateka mataifa mawili ya Iran na Iraq na kurejea vikosi vya nchi mbili hizo katika mipaka ya kimataifa. Utawala vamizi wa Iraq hapo kabla ulikuwa umelikubali azimio hilo na ulikuwa ukiendesha propaganda dhidi ya Iran kutokana na kutolikubali azimio hilo. Lakini wakati Iran pia ilipotangaza kulikubali azimio hilo, jeshi la dikteta Saddam kwa mara nyingine tena likaishambulia ardhi ya Iran. ***
