Jul 22, 2025 03:17 UTC
  • Jumanne, Julai 22, 2025

Leo ni Jumanne tarehe 26 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria sawa na Julai 22, 2025.

Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita mji mtakatifu wa Makka ulishambuliwa kwa mawe ya moto baada ya kuzingirwa na jeshi la mtawala mal'uni wa kizazi cha Bani Umayyah, Yazid bin Muawiya.

Baada ya kumuua shahidi Imam Hussein na wafuasi wake katika jangwa la Karbala na Watu wa Nyumba ya Mtume wakachukuliwa mateka, Yazid alidharaulika sana na kukosa heshima katika Umma wa Kiislamu. Waislamu katika maeneo mbalimbali walianzisha uasi dhidi ya utawala wake. Harakati hizo za uasi zilifika hadi Hijaz hapo mwaka 63 Hijria ambapo watu wa Makka walimfukuza gavana wa Yazid na kuchukua madaraka ya mji huo. Mtawala huyo alituma jeshi ambalo liliuzingira mji huo mtukufu na kushambulia Msikiti wa Makka na al Kaaba kwa mawe ya moto.   

Miaka 424 iliyopita aliaga dunia Sheikh Abdullah Tostari faqihi na msomi wa Kiislamu wa Kiirani.

Sheikh Tostari alifikia daraja ya ijtihad baada ya kuhitimu masomo ya kidini chini ya maustadhi wakubwa wa zama hizo. Sheikh Abdullah Tostari baadaye alielekea katika hauza ya kielimu ya mji wa Isfahan nchini Iran na kuanza kufundisha masomo ya dini. Darsa ya mujtahidi huyo ilikuwa ikihudhuriwa na wanafunzi wengi ambao walinufaika na bahari kubwa ya elimu yake.

Allamah Majlisi na Mirza Muhammad Naini ni miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Abdullah Tostari.   

Miaka 412 iliyopita katika siku kama ya leo, Mikhail Ramanov alikalia kiti cha utawala wa Russia na kwa utaratibu huo, utawala wa miaka 304 wa familia ya Ramanov ukawa umeanza nchini humo.

Miaka mitatu baada ya mashambulio ya vikosi vya Poland dhidi ya Russia, mmoja wa makamanda wa Kirusi alifanikwa kuvishinda vikosi hivyo na kuudhibiti mji wa Moscow. Baada ya jeshi la Poland kufukuzwa nchini humo, Mikhail Ramanov akashika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Katika kipindi cha utawala wa familia ya Ramanov, Russia ilipanuka lakini kwa upande wa uchumi haikupiga hatua kubwa.   

Mikhail Ramanov

Katika siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, kulitokea vita maarufu vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Isonzo.

Vita hivyo vilitokea sambamba na kujiri Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Vita vya Isonzo vilitokea katika maeneo ya milimani yaliyojulikana kwa jina hilo hilo nchini Italia.

Vita hivyo vilikuwa baina ya jeshi la Italia lililokuwa katika safu ya waitifaki na Austria iliyokuwa upande wa Ujerumani. Watu wapatao 70,000 wengi wao wakiwa ni Wataliano waliuliwa katika vita vyab Isonzo. Pamoja na hayo, jeshi la Italia lilipata ushindi dhidi ya jeshi la Austria katika vita hivyo. 

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Julai 1961, yalianza mapigano makali kati ya majeshi ya Ufaransa na Tunisia, baada ya vikosi vya Ufaransa kuushambulia mji wa kihistoria wa Bizerte ulioko kaskazini mashariki mwa Tunisia.

Mara baada ya Tunisia kujitawala kutoka kwa mkoloni Mfaransa mwaka 1956, mkoloni huyo aliendelea kuikalia kwa mabavu bandari ya Bizerte, na kuifanya kuwa kambi ya jeshi la anga la nchi hiyo.

Hata hivyo majeshi ya Tunisia yalifanikiwa kuikomboa bandari hiyo kwenye mapigano hayo makali yaliyopelekea Watunisia 750 kuuawa.

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, jeshi la mtawala wa wakati huo wa Iraq, dikteta Saddam Hussein lilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya maeneo ya kusini ya Iran.

Mashambulio hayo yalianza siku nne tu baada ya Iran kulikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lililokuwa limepasishwa takribani mwaka mmoja kabla, lilisisitiza juu ya usitishaji vita, liliuarifisha  utawala vamizi, likataka kulipwa fidia waathiriwa wa hujuma hiyo, kubadilishana mateka mataifa mawili ya Iran na Iraq na kurejea vikosi vya nchi mbili hizo katika mipaka ya kimataifa.

Utawala vamizi wa Iraq hapo kabla ulikuwa umelikubali azimio hilo na ulikuwa ukiendesha propaganda dhidi ya Iran kutokana na kutolikubali azimio hilo. Lakini wakati Iran pia ilipotangaza kulikubali azimio hilo, jeshi la dikteta Saddam kwa mara nyingine tena likaishambulia ardhi ya Iran.

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, ndege za kivita za utawala wa Israel zilishambulia eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina, na kuua watu 16 na wengine 150 kujeruhiwa.

Shambulio hilo la kushtukiza lililofanyika usiku, liliua watoto 9 wasiokuwa na hatia yoyote. Hali kadhalika miongoni mwa waliouawa shahidi katika shambulizi hilo ni Sheikh Swalah Shahadah, mmoja wa makamanda wa Brigedi ya Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya kiislamu ya Palestina HAMAS ambaye aliuawa akiwa pamoja na mkewe na binti yake. 

Sheikh Swalah Shahadah

Miaka 22 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 22 Julai 2003, waliuawa Uday na Qusay watoto wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq pambizoni mwa mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq.

Uday na Qusay wakiwa wamefuatana na maafisa wa ngazi za juu wa Iraq walitoroka mjini Baghdad baada ya majeshi ya Marekani na Uingereza kuishambulia nchi hiyo mwezi Aprili 2003.

Majeshi ya Marekani yalishambulia nyumba walimokuwa wamejificha watoto hao wa Saddam Hussein na kuwauwa pamoja na wasaidizi wao.

Uday na Qusay watoto wa Saddam