Jumapili, 27 Julai, 2025
Leo ni Jumapili tarehe Pili Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria mwafaka na 27 Julai 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1326 iliyopita, aliuawa shahidi Zaid bin Ali bin Hussein mwana wa Imam Sajjad (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Zaid bin Ali alisimama kupambana na dhulma za Banii Umayyah na kulinda matunda ya mapambano ya babu yake, Imam Hussein bin Ali (as). Baada ya mapambano ya kishujaa, Zaid bin Ali aliuawa shahidi katika mji wa Kufa nchini Iraq. Harakati ya mapambano ya Zaid ni miongoni mwa matunda ya mapambano ya Imam Hussein (as) katika medani ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria kwani baada ya mapambano ya siku ya Ashuraa kulijitokeza harakati nyingi baina ya Waislamu zilizopigana jihadi kwa lengo la kuuondoa madarakani utawala dhalimu wa Banii Umayyah.
Siku kama yale leo miaka 1177 iliyopita, sawa na tarehe pili Safar mwaka 270 Hijiria, harakati ya mapambano za Wazanji ilifeli baada ya kuuawa kiongozi wa harakati hiyo Sahib al-Zanj. Ali Bin Muhammad maarufu kwa jina la Sahib al-Zanj ambaye alikuwa akijitambua kuwa mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) na Imam Ali bin Abi Twalib (as) alianzisha harakati ya mapambano mwaka 255 Hijiria akisaidiwa na wafuasi wake pamoja na watumwa weusi ambao walikuwa wakiitwa Wazanji, dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Bani Abbas huko kusini mwa Iraq. Sahib al-Zanj aliwaahidi watumwa hao weusi kuwaachilia huru kutoka katika minyororo ya utumwa na kuwapa haki zao za kijamii kama watu wengine suala ambalo liliwafanya watu wa jamii hiyo kuvutiwa na harakati yake. Mwaka 257 Sahib al-Zanj aliudhibiti mji muhimu wa Basra, Iraq na taratibu akaanza kutwaa maeneo mengine ya karibu na mji huo. Katika kipindi hicho majeshi ya utawala wa Bani Abbasi yalifanya hujuma kadhaa dhidi ya Wazanji lakini hata hivyo hujuma hizo zilifeli kutokana na msimamo imara wa jamii ya watu hao weusi. Hata hivyo kutokana na matatizo ya ndani Wazanji walidhoofika sana na harakati yao iliyoendelea kwa kipindi cha miaka 15 ikasambaratika baada ya kuuawa kiongozi wao Sahib al-Zanj.
Siku kama ya leo miaka 702 iliyopita, alifariki dunia nchini Misri, Abu Hayyan Gharnatwi, malenga na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 654 Hijiria huko Andalusia 'Uhispania ya leo' na baadaye alifanya safari katika miji mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Mwaka 679 Abu Hayyan Gharnatwi, alielekea nchini Misri ambako aliishi hadi mwisho wa maisha yake. Akiwa nchini humo alijishughulisha na ufundisha na kuandika vitabu. Gharnatwi alikuwa mtaalamu wa elimu ya Qur'ani, Hadithi na sharia za Kiislamu, lakini alipata umashuhuri mkubwa katika utaalamu fasihi ya lugha ya Kiarabu. Abu Hayyan Gharnatwi ambaye mwishoni mwa uhai wake alikuwa kipofu, ameacha turathi nyingi kama kitabu cha 'Al-Idraaku Lilisaanil-Atraak' 'Tadhkiratun-Nuhaat' 'Tafsirul-Bahril-Muhit' na diwani ya mashairi.

Miaka 253 iliyopita, katika siku kama ya leo ulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kuigawa Poland kati ya madola matatu makubwa ya Ulaya katika karne ya 18. Poland ambayo hii leo ni moja ya nchi zilizo huru za mashariki mwa Ulaya, iligawanywa baina ya nchi tatu za Urusi, Austria na Prusssia kwa kutiwa saini makubaliano yaliyotajwa. Ni muhimu kuashiria hapap kwamba hadi sasa Poland imeshawahi kugawanywa mara nne kati ya nchi tofauti.

Miaka 201 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas. Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa. ***

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 5 Mordad mwaka 1358 Hijria Shamsiya, iliswaliwa rasmi Swala ya kwanza ya Ijumaa katika mji wa Tehran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Tehran ikiongozwa na marehemu Ayatullah Talaqani, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu, kufuatia agizo la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Swala ya Ijumaa haikuwa ikifanyika kutokana na kuweko anga ya udhibiti na ukandamizaji wa serikali ya Shah.

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi mfalme wa mwisho wa Iran aliaga dunia huko Cairo, Misri. Aliingia madarakani baada ya baba yake yaani Rezakhan kuondolewa kwenye uongozi na kubaidishwa na Waingereza. Kama alivyokuwa baba yake, Muhammad Reza Pahlavi alikuwa na uhusiano mkubwa na Uingereza na ndio maana akafanya jitihada za kulinda maslahi haramu ya nchi hiyo nchini Iran. Hata hivyo baada ya harakati za wananchi na kushinda harakati ya kuitaifisha sekta ya mafuta, maslahi ya Waingereza nchini Iran yalifikia tamati. Shah aliwakandamiza wananchi wa Iran kwa ngumi ya chuma na alikuwa kibaraka mkubwa wa Marekani. Suala hilo lilizidisha kasi ya harakati za Mapinduzi ya Kiislamu zilizoongozwa na hayati Imam Khomeini na mwaka 1357 Mapinduzi ya Kiislamu yalihitimisha utawala dhalimu wa Shah ambaye alikimbilia nje ya nchi na kufia Misri katika siku kama hii ya leo.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, ilianza operesheni kubwa ya kijeshi iliyopewa jina la "Mirsad" huko magharibi mwa Iran kwa lengo la kuwasambaratisha vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqin. Kundi la Munafiqin ambalo lilikuwa limekusanya magaidi katika mpaka wa Iran na Iraq wakiwa na silaha nzito kutoka kwa utawala wa zamani wa Baghdad lilianza kuishambulia ardhi ya Iran siku mbili kabla ya kuanza operesheni hiyo. Kiongozi wa Munafiqin alidhani kuwa magaidi hao wangeweza kuvuka barabara kuu za Iran bila ya kizuizi na tabu yoyote na kufika haraka mjini Tehran. Hata hivyo wanajeshi wa Iran wakishirikiana na wananchi waliojitolea katika operesheni hiyo ya Mirsad waliwazingira vibaraka hao wa Munafiqin huko magharibi mwa nchi na kuwasambaratisha magaidi hao walio na uhusiano mkubwa na nchi za kigeni.
