Leo Jumatatu, tarehe 28 Julai, mwaka 2025
Leo ni tarehe tatu Safar 1447 Hijria sana na Julai 28 mwaka 2025.
Miaka 1390 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Mwezi 3 Safar mwaka 57 Hijria Qamaria, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, alizaliwa Imam Muhammad Baqir (AS), mjukuu kipenzi wa Bwana Mtume SAW katika mji wa Madina,.
Ukamilifu wa kiroho na kielimu ambayo ni hidaya ya Mwenyezi Mungu waliyotunukiwa Ahlubaiti wa Mtume SAW, ulidhihirika kwa uwazi katika shakhsia ya Imam Muhammad Baqir (AS). Katika kipindi cha miaka 19 ya Uimamu wa mtukufu huyo, ambacho kilisadifiana na miaka ya mwishoni ya utawala wa Bani Umayyah, yalipatikana mazingira mwafaka katika jamii kwa yeye kuweza kuimarisha misingi ya kifikra na kiutamaduni ya Waislamu. Taaluma nyingi zilistawishwa na kuenea katika jamii ya Waislamu kupitia chuo cha fikra cha mtukufu huyo pamoja na mwanawe, yaani Imam Ja'far Sadiq (AS); na hata wanafunzi wake walikuja kuwa wavumbuzi wa taaluma mbalimbali mpya za elimu.
Lakini sambamba na hayo, Imam Baqir hakughafilika na kupambana na dhulma na uonevu wa utawala wa kidhaliimu wa Bani Umayyah na ndiyo maana katika mwaka 114 Hijria Qamaria aliuliwa shahidi na mtawala wa zama hizo. Tunachukua fursa hii pia kukupeni mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa kuadhimisha kuzaliwa kwa mjukuu huyo kipenzi wa Mtume SAW.

Tarehe 28 Julai miaka 296 iliyopita harakati ya kwanza ya mapambano ya watumwa weusi wa Marekani ilianza huko kaskazini mwa nchi hiyo.
Waanzilishi wa harakati hiyo ambao walikuwa watu 44 walimuua kila mzungu waliyekutana naye katika njia yao kutoka Carolina Kusini kuelekea Florida. Lakini walizingirwa na jeshi la Waingereza na kuuawa kabla ya kuingia Florida na kupata uhuru.
Baada ya hapo watumwa weusi waliendeleza mapambano ya ukombozi na kupigania haki zao za kiraia. Watumwa weusi walikuwa wakitekwa nyara au kununuliwa kutoka Afrika tangu mwanzoni mwa karne ya 17 na kupelekwa Marekani kwa ajili ya kuuzwa na kufanyishwa kazi kwa mabwana zao.

Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, nchi ya Peru ilijipatia uhuru na siku hii hutambuliwa kuwa ni siku ya kitaifa nchini humo.
Peru ilikuwa sehemu ya asili ya watu waliostaarabika wa Inca na tokea karne ya 12 hadi ya 16 ufalme wa watu hao ndio uliotawala kaskazini magharibi mwa Amerika ya Kusini. Mwanzoni mwa karne ya 16 wakoloni wa Uhispania waliingia Peru na baada ya mauaji ya kikatili dhidi ya Wahindi wekundu hatimaye ardhi ya Peru ikatawaliwa na wakoloni wa Uhispania.
Wahispania waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi hiyo sambamba na kupora mali na raslimali za watu wa Peru hali iliyopelekea kupamba moto mapinduzi ya wapigania uhuru nchini humo. Peru iko kaskazini magharibi mwa Amerika ya Kusini, huku ikipakana na nchi za Ecuador, Colombia, Chile, Brazil na Bolivia.

Katika siku kama ya leo miaka 147 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Barlin, mwishoni mwa kongamano lililofanyika mjini humo kati ya wajumbe wa nchi za Russia, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Austria.
Mkutano wa Berlin ulifanyika kwa ombi la kansela wa wakati huo wa Ujerumani, Otto Von Bismarck. Kutiwa saini mkataba huo kuliifanya Ujerumani kuwa na satua ya kisiasa na kijeshi na kuandaa uwanja wa kujitanua zaidi nchi hiyo. Kimsingi kutiwa saini mkataba huo wa Berlin kulikuwa moja ya mambo yaliyoandaa uwanja wa kutokea Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.

Miaka 111 iliyopita, wakati wa kukaribia kuanza Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa kifalme wa Austria ulitangaza vita dhidi ya serikali ya Serbia kwa kisingizio cha kuuawa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo huko Serbia.
Hata hivyo sababu kuu ya kutolewa tangazo hilo la vita ilikuwa upinzani wa wananchi wa Serbia dhidi ya uingiliaji wa Austria katika masuala ya ndani ya nchi yao na pia kufanyika uasi dhidi ya nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, tetemeko kubwa liliukumba mji wa Tangshan mashariki mwa China.
Tetemeko hilo ambalo lilikuwa na ukubwa wa rishta 7.8, lilipelekea kuuawa watu wapatao laki sita na malaki kadhaa ya wengine kujeruhiwa sambamba na kuwa wakimbizi. Hata hivyo ripoti rasmi iliyotangazwa na viongozi wa China ilionyesha kuwa, idadi ya watu waliouawa katika tetemeko hilo ilikuwa laki mbili na 40 elfu.
Hilo lilikuwa tetemeko kubwa zaidi kuwahi kuikumba China katika karne ya 20 na tetemeko kubwa kushuhudiwa tangu tetemeko la mwaka 1556 ambalo lilipelekea kuuawa kwa watu laki nane na elfu 30.
